• HABARI MPYA

    Monday, August 24, 2015

    MALAIKA BAND, FM ACADEMIA MLIJITATHMINI AU MLIKURUPUKA?

    IJUMAA iliyopita kulikuwa na manyesho mawili makubwa ya muziki wa dansi, upande mmoja FM Academia na upande wa pili Malaika Music Band.
    FM walikuwa East 24 Arcade House Mikocheni wakisherehekea miaka 18 ya uhai wa bendi yao pamoja na utambulisho wa nyimbo mbili mpya.
    Malaika wao walikuwa Mango Garden Kinondoni wakitambulisha audio na video ya wimbo wao mpya “Amerudi” huku onyesho hilo likija hapo Mango baada ya kutoonekana kwa zaidi ya miezi miwili ndani ya ukanda wa Kinondoni.
    Katika kipindi hiki ambacho muziki wa dansi umepotoea, halafu yakagongana maonyesho mawili makubwa - tena ndani ya eneo la Kinondoni na vitongoji vyake ambalo ndilo linaloenekana kama mwokozi wa muziki huo, linakuwa si jambo la kuvutia sana.
    Sina haja ya kusema bendi gani ilikosea au bendi gani ‘ilimfuata’ mwenzie ila ni wazi kuwa kugongana kwa maonyesho hayo kulipelekea usumbufu mkubwa kwa mashabiki wa muziki wa dansi, wengi wao wakalazimika kujigawa huku na huku na kuhakikisha wanatia timu katika kumbi zote mbili.
    Hiyo maanake nini? Maana yake ni kwamba mtu mmoja analazimika kutumia gharama kubwa zaidi lakini wakati huo huo anakuwa na hasara ya kushuhudia nusu tu ya kila onyesho. 
    Bendi zote mbili zikalazimika kuongeza nguvu ya matangazo  pengine kuliko ambavyo ingekuwa kama maonyesho hayo yasingegongana.
    FM Academia na Malaika zikafanikiwa kuzoa mashabiki wengi, lakini ni ukweli usiopingika kuwa ipo moja wapo miongoni mwa bendi hizo ambayo iliathirika kwa kugongana kwa maonyesho hayo.
    Ni bendi gani iliyo kuwa mbabe kati ya Malaika na FM Academia? Ipi ilipata faida? Ipi ilichungulia mlango wa hasara?
    Ni Malaika Band iliyobebwa zaidi na uwezo na nyota ya Christian Bella au FM Academia inayojengwa zaidi kitimu kwa kutegemea wanamuziki waliokaa pamoja kwa muda mrefu?
    Mimi sina jibu wala sitaki kuwa mwamuzi, waamuzi ni wale wakereketwa wa kweli waliohakikisha wanachungulia maonyesho yote mawili.
    Najiuliza sana, hivi ilikuwepo kweli haja ya bendi hizi mbili kufanya maonyesho makubwa ndani ya siku moja? Viongozi wa bendi hizi hawakuwa na uwezo wa kukaa meza moja na kutatua jambo hili? Wana uadui? Ni chembechembe za kisasi? Ni mambo ya muosha huoshwa?
    Miaka nane iliyopita bendi ya Akudo Impact chini ya Christian Bella ilifanya onyesho kubwa la utambulisho wa albam ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee, lakini FM Academia nao wakaibuka na onyesho la miaka 1o ya bendi ndani ya New Msasani Club kwa siku hiyo hiyo na ili kuteka mashabiki wakamwalika Defao …mbona ilikuwa patashika mjini.
    Haya ni matendo ambayo hayapaswi kuachwa yapite hivi hivi  bila kukemewa, kwa mara nyingine tena nasisitiza viongozi wa muziki wa dansi na taarab anzisheni mfumo (Network) ambao utawasaidia japo kupeana kalenda za maonyesho yenu.
    Kwa kuanzia mnaweza mkawa japo na group lenu la Whatsapp litakalokuwa na angalau viongozi watatu kutoka kila bendi, ambapo humo sasa ratiba zenu zote zitakuwa hadharani na huo utakuwa mwanzo mzuri wa kuepuka migongano kama hiii iliyotokea kwa FM Academia na Malaika Band.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALAIKA BAND, FM ACADEMIA MLIJITATHMINI AU MLIKURUPUKA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top