• HABARI MPYA

  Jumanne, Julai 24, 2018

  ULIMWENGU AENDELEA KUNG’ARA SUDAN…JANA AMEFUNGA PIA AL HILAL IKISHINDA 4-0 LIGI YA SUDAN

  Na Mwandishi Wetu, PORT SUDAN
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu jana ameendelea kung’ara nchini Sudan baada ya kufunga bao moja katika ushindi wa timu yake, Al Hilal Omdurman wa 4-0 dhidi ya Hay Al Arab kwenye Ligi Kuu ya Sudan.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Port Sudan, Ulimwengu alianza na kucheza vizuri kiais cha kukaribia kufunga bao lingine.
  Huo unakuwa ushindi wa pili mfululizo katika mechi zote mbili za mwanzo za Ligi Kuu ya Sudan unaoiweka kileleni Al Hilal kwa pointi zake sita, huku Ulimwengu akifunga katika mechi zote hizo.
  Ulimwengu alifunga pia Julai 18 Al HIlal ikitoka sare ya 2-2 na Songo ya Msumbiji katika mchezo wa Kundi B Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Al-Hilal mjini Omdurman.

  Ikumbukwe, Ulimwengu amejiunga na El Hilal mwishoni mwa mwezi Mei baada ya kuachana na AFC Eskilstuna ya Sweden ambayo alishindwa kuitumikia vyema kutokana na kuandamwa na maumivu ya goti yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya Taasisi ya Sayansi ya Michezo mjini Cape Town, Afrika Kusini mwaka jana na kupitia kipindi kirefu cha mazoezi ya kujiweka fiti.
  Ulimwengu alikwenda kwa watalaamu nchini Italia kufanyishwa mazoezi maalum ya kumuweka fiti haraka arejee uwanjani, ambayo hakika yamemsaidia hadi kuanza vyema na vigogo wa Sudan.
  Maumivu ya goti yalikuwa yakimsakama Ulimwengu tangu alipojiunga na Eskilstuna Januari mwaka jana akitokea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kiasi cha kushindwa kucheza. 
  Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011  alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
  Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
  Ulimwengu alihamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ULIMWENGU AENDELEA KUNG’ARA SUDAN…JANA AMEFUNGA PIA AL HILAL IKISHINDA 4-0 LIGI YA SUDAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top