• HABARI MPYA

    Monday, July 30, 2018

    EDDY JUAN FRANCIS NA MANA NAKAO MABEKI WA TANZANIA WANAOTAMBA LIGI KUU ZA CHINA NA JAPAN

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI Yussuf Yussuf Yurary Poulsen alikuwa mjadala mkubwa kwa wadau wa soka nchini Tanzania wakati wa fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi kati ya Juni na Julai mwaka huu.
    Hiyo ni kutokana na mchezaji huyo kuonyesha nia ya kuchezea Tanzania awali, nchi ya baba yake, lakini akapuuzwa hadi akachukuliwa na Denmark aliyoichezea kwenye fainali za Urusi.
    Yussuf Poulsen aliyezaliwa Juni 15, mwaka 1994 ambaye kwa sasa anachezea RB Leipzig ya Ujerumani kama winga na mshambuliaji, baba yake marehemu kwa sasa ni Mtanzania na mama yake ni Mdenmark.
    Baba yake alikuwa baharia wa Melini kwa safari za Tanga na Denmark kabla ya kuamua kuhamia mjini Copenhagen ambako ndiko umauti ulimkuta.
    Alifariki kwa ugonjwa wa saratani wakati Yussuf akiwa ana umri wa miaka minne tu. Yussuf amekuwa akizuru Tanzania mara kadhaa tangu mwaka 1996 akiwa mdogo na baadaye mwaka 2002, 2008 na 2011 mara ya mwisho. 
    Yussuf hakuwa hata mara moja kuitwa timu ya taifa ya Tanzania na ndiyo maana akachagua kuchezea Denmark nchi ya mama yake.
    Kwa makosa hayo, Mkurugenzi wa Michezo, Dk. Yusuphu Singo akawaagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wafuatilie vipaji vya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza nje.
    Na wakati TFF bado wanalifanyia kazi agizo la Serikali, Bin Zubery Sports – Online imewapata wachezaji wengine wawili wenye asili ya Tanzania wanaocheza nje, ambao ni mabeki, Eddy Juan Francis anayechezea Shanghai Shenhua ya Ligi Kuu ya China na Mana Nakao anayechezea AS Laranja Kyoto ya Ligi Kuu ya Japan.
     Eddy Juan Francis wakati anatangazwa kujiunga na Shanghai Shenhua ya Ligi Kuu ya China

    EDDY JUAN FRANCIS 
    Eddy Juan Francis aneyefahamika zaidi kama Aidi Fulangxisi, alizaliwa mjini Shanghai, Desemba 17 mwaka 1990 mama yake akiwa ni Mchina na baba yake Mtanzania. 
    Kisoka aliibukia katika akademi ya Genbao (GFA) akiwa ana umri wa miaka 10 tu kabla ya mwishoni mwa mwaka 2005 kujiunga na Shanghai East Asia. 
    Lakini baada ya msimu wake wa kwanza, aliteremshwa na kupelekwa Shanghai Shenhua na mwaka 2008 akaenda kujiunga na klabu ya Daraja la Pili China, Suzhou Trips ambako hata hivyo hakucheza kutokana na matatizo katika usajili wake. 
    Mwaka 2009 Suzhou Trips ikajitoa kwenye Ligi ya China na Eddy akasaini kwa mkopo wa mwaka mmoja, Ningbo Huaao. Alipomaliza mkopo wake, akahamia Ligi Daraja la Kwanza China, akirejea Shanghai East Asia.
    Januari 20 mwaka 2012, Shanghai East Asia ikabadilishana Eddy na Luis Cabezas wa timu ya Ligi Kuu China, Dalian Aerbin. Alirudishwa kwa mkopo wa mwaka mmoja Shanghai East Asia Februari mwaka 2012, ambako kwa mara nyingine akashindwa kupata nafasi, akiishia kucheza mechi tatu tu tena zote akitokea benchi msimu wa 2012. 

    Eddy Juan Francis akimdhibiti mshambuliaji wa timu pinzani katika moja ya mechi alizocheza China

    Machi 8, mwaka 2014, Eddy akacheza mechi yake ya kwanza Dalian Aerbin katika msimu wa 2014 wa Ligi Kuu ya China dhidi ya Hangzhou Greentown, akitokea benchi kwenda kuchukua nafasi ya Zhu Xiaogang dakika ya 77.
    Januari 29, mwaka 2017, klabu ya Boavista ya Ureno ikamsajili Eddy kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu kutokana na uhusiano baina yao na Chama cha Soka China.
    Na Februari 7, mwaka 2018, Shanghai Greenland Shenhua ikatangaza kumchukua Eddy na kumsajili katika Ligi Kuu ya China na Ligi ya Mabingwa Asia msimu huu.
    Eddy aliichezea kwa dakika 27 tu timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 14 ya China kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Asia kwa vijana wa umri wa huo mwaka 2004 (AFC U-14 Championship) na sasa anawania kuingia kwenye kikosi cha timu ya taifa yawakubwa ya China baada ya kuoma nchi yake ya asili, Tanzania haijammulika.
    Mana Nakao anachezea AS Laranja Kyoto ya
    Ligi Kuu ya Japan

    MANA NAKAO
    Mana Nakao naye alizaliwa Septemba 2, mwaka 1986 mjini Uji, Kyoto nchini Japan, naye kama Yussuf na Eddy, baba yake ni Mtanzania na mama yake ndiye Mjapan.
    Kwa sasa anachezea AS Laranja Kyoto ya Ligi Kuu ya Japan baada ya awali kuchezea timu mbalimbali za nchini humo tangu akiwa kijana mdogo kabisa.
    Aliibukia Sanfrecce Hiroshima alikocheza kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 alipohamia Zweigen Kanazawa ambako baada ya mechi 14, akahamia AS Laranja Kyoto mwaka 2009 ambako hadi sasa amekwishacheza mechi 83 na kufunga mabao 15.
    Akiwa beki mkongwe kwa sasa anayemalizia maisha yake ya soka anaweza kusaidia nchi yake ya asili Tanzania japo kwa muda mfupi kwenye mashindano ya kimataifa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: EDDY JUAN FRANCIS NA MANA NAKAO MABEKI WA TANZANIA WANAOTAMBA LIGI KUU ZA CHINA NA JAPAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top