• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 23, 2018

  SIMBA SC WAANZA KUJIFUA UTURUKI CHINI YA KOCHA MPYA MBELGIJI PATRICK AUSSEMS

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Simba SC kimewasili salama mjini Istanbul, Uturuki leo baada ya kuondoka Aflajiri ya Jumapili kuweka kambi ya muda wa wiki mbili kujiandaa na Ligi Kuu ya Tanzania bara inayotarajiwa kuanza Agosti 22, mwaka huu.
  Na mara baada ya kuwasili, Simba SC walipumzika kidogo kabla ya kwenda kufanya mazoezi yao ya kwanza jioni ya leo Istanbul ambayo pia yalikuwa mazoezi ya kwanza chini ya kocha mpya, Mbelgiji Patrick J Aussems. 
  Simba SC imeondoka na wachezaji wote iliyowasajili kwa ajili ya msimu ujao chini ya kocha wake mpya Aussems atakayekuwa chini ya Msaidizi Mrundi, Masoud Juma aliyekuwa Msaidizi pia wa makocha wawili waliopita, Mcameroon Joseph Omog na Mfaransa, Pierre Lechantre.
  Kocha mpya wa Simba SC, Mbelgiji Patrick J Aussems (kulia) akizungumza na wachezaji 
  Patrick J Aussems (kulia) akizungumza na wachezaji wa Simba leo mjini Istanbul  
  Wachezaji wa Simba SC wakiwa kwenye ndege wakati wa safari ya Uturuki 

  Beki Muivory Coast, Serge Wawa Pascal (kulia) leo wamekutana tena uwanjani na kipa Aishi Manula baada ya kuachana Azam FC miaka miwili iliyopita

  Ikiwa nchini Uturuki, Simba SC itapata mazoezi katika mazungira na viwanja bora, pamoja na mechi za kirafiki za kujipima nguvu kabla ya kurejea nchini kwa ajili ya tamasha la Simba Day Agosti 8 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Ikumbukwe Simba SC, mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania watauanza msimu kwa mchezo wa wa Ngao ya Jamii dhidi ya washindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu Azam Sports Federation Cup (ASFC), Mtibwa Sugar Agosti 18, mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.               
  Katika Ligi Kuu, Simba itaanza na Tanzania Prisons Agosti 22, mechi itakayochezwa Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Na watakutana na mahasimu wao wa jadi, Yanga watakutana Septemba 30, mwaka huu katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAANZA KUJIFUA UTURUKI CHINI YA KOCHA MPYA MBELGIJI PATRICK AUSSEMS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top