• HABARI MPYA

    Thursday, July 26, 2018

    NAIBU WAZIRI SHONZA KUWA MGENI RASMI SIKU YA UREMBO WA ASILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, atakuwa mgeni rasmi katika tamasha la kwanza la siku ya urembo wa nywele na ngozi za asili litakalofanyika Julai 28, mwaka huu viwanja vya Makumbusho ya Taifa yaliyopo Posta, Dar es Salaam.
    Onyesho hilo ambalo litaanza saa tatu asubuhi limeandaliwa na kampuni ya Eagle Business Consultants ya jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwahamasisha wanawake wa Kiafrika kuthamini urembo wao wa asili na kuachana na tabia ya kuutukuza utamaduni wa kimapokezi wa kubadilisha mwonekano wao.
    Kwa mujibu wa mmiliki na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya Eagle, Antu Mandoza, onesho hili litakuwa likifanyika kila mwaka na kuifanya tarehe hii kuwa Siku ya Urembo wa Asili kwa kuanzia na Tanzania na baadaye Afrika Mashariki na hatimaye bara zima la Afrika.


    Naibu Waziri, Juliana Shonza atakuwa mgeni rasmi siku ya urembo wa nywele na ngozi za asili Julai 28 

    Mandoza ameeleza pia kwamba onesho hili linalenga kutoa elimu kwa jamii nzima kuhusu madhara ya kiafya ya kutumia kemikali za aina mbalimbali za urembo wa nywele na uchubuaji ngozi ili kurejesha ujasiri wa zamani wa mwanawake wa Afrika wa kujiamini na kupenda asili yake.
    Mandoza alianza kampeni ya urembo wa asili kwa kupitia kwenye mitandao ya kijamii mnamo Machi 2018 ambapo amekuwa akitumia utambulisho au hashtag ya naturalhairsioushamba. Kampeni hii iliungwa mkono na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
    Mwitikio mzuri wa kampeni ya mtandaoni ndio uliopelekea kuzaliwa kwa wazo la kuandaa onesho hili maalumu linalotarajiwa liwe mkombozi wa kizazi kijacho cha Afrika kwa baraka za serikali kupitia kwa Naibu Waziri Shonza.
    Onesho hili litahudhuriwa na wasanii, wanamitindo na wataalamu mbalimbali akiwemo Dkt. Andrew Foi ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi atakayetoa mada kuelezea madhara ya kutumia kemikali katika urembo na kutoa siri za kuboresha nywele na ngozi kwa kutumia vitu vya asili. Hakutakuwa na kiingilio chochote na wananchi wote wanakaribishwa.
    Kampuni ya Eagle pia inamiliki redio ya mtandaoni iitwayo radio7 www.radio7.co.tz ambayo huelimisha pamoja na kuiburudisha jamii.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NAIBU WAZIRI SHONZA KUWA MGENI RASMI SIKU YA UREMBO WA ASILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top