• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 30, 2018

  AKINA SAMATTA WAANZA NA MOTO MSIMU MPYA LIGI KUU UBELGIJI…WAWAPIGA WAPINZANI 4-0

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana ameisaidia timu yake, KRC Genk kuifunga mabao 4-0 Sporting Lokeren katika mchezo wa kwanza wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Daknamstadion mjini Lokeren.
  Samatta jana hakufunga wala kutoa pasi ya bao, lakini alikuwa ana mchango mkubwa kwenye ushindi huo, kutokana na ulinzi mkali wa mabeki wawili wa Lokeren aliowekewa na kuwapa mwanya wachezaji wengine kufunga kwa urahisi.
  Mabao ya Genk jana yalifungwa na kiungo Mspaniola, Alejandro Pozuelo dakika ya tatu, kiungo wa Ukraine Ruslan Malinovskiy dakika ya 16, mshambuliaji Mkongo, Dieumerci N'Dongala dakika ya 61 na mshambuliaji Mbelgiji, Leandro Trossard dakika ya 73. 
  Mshambuliaji wa KRC Genk, Mbwana Samatta akimiliki mpira mbele ya mchezaji wa Lokeren jana  
   
  Huo ulikuwa ni mchezo wa 99 kwa Samatta kuichezea KRC Genk kwenye mashindano yote na mechi za kirafiki akiwa amefunga mabao 26 tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambayo ilimtoa Simba SC ya Tanzania mwaka 2011.
  Samatta hakuwa na msimu mzuri sana uliopita baada ya kuumia goti Novemba 4, mwaka jana akiichezea KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk na kukaa nje hadi Februari mwaka huu huku ikimchukua hadi Aprili kuanza kuonyesha makali tena.
  Samatta alichanika mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia akiichezea mechi ya 70 Genk tangu alipojiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na alipopona akacheza mechi 20 zaidi, ingawa nyingi alitokea benchi. 
  Kikosi cha Sporting Lokeren; Verhulst, Marzo, Maric, Skulason, Overmeire, Cevallos/Diaby dk71, Miric/Hupperts dk45, De Ridder, Marecek/Terki dk79, Filipovic na Saroka.
  KRC Genk; Vukovic, Uronen, Dewaest, Aidoo, Maehle/Nastic dk51, Berge/Seck dk73, Malinovskyi, Pozuelo/Gano dk84, Trossard, Ndongala na Samatta.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AKINA SAMATTA WAANZA NA MOTO MSIMU MPYA LIGI KUU UBELGIJI…WAWAPIGA WAPINZANI 4-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top