• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 29, 2018

  YANGA SC WADAI TFF IMEWAFUNGISHA KWA GOR MAHIA LEO…ILIONDOA NYOTA SITA KAMBINI JANA MCHANA NA KUWARUDISHA USIKU WA MANANE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Msaidizi wa Yanga SC, Mzambia Noel Mwandila amelalamikia kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwaondoa wachezaji wao sita kambini jana mchana na kuwarudisha usiku wa manane kwamba kimechangia wao kupoteza mechi dhidi ya Gor Mahia leo.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya mchezo huo, Mwandila aliwataja wachezaji hao kuwa ni kipa Ramadhani Kabwili, beki Gardiel Michael na viungo Raphael Daudi, Gardiel Michael, Ibrahim Ajib na Deus Kaseke.
  Mwandila alisema Mkurugenzi wa Masoko wa TFF, Aaron Nyanda aliondoka na wachezaji hao saa 8:00 hoteli ya Zimbo, iliyopo makutano ya mitaa ya Ndovu na Nyamwezi na kuwarudisha baada ya Saa 8:00 usiku.

  Noel Mwandila (kushoto) amelalamikia kitendo cha TFF kuwaondoa wachezaji wao sita kambini jana 

  Pamoja na kumkatalia kwa sababu timu ilikuwa ina mechi leo, lakini Mwandila amesema Nyanda alisistiza kuwachukua kwa sababu walikuwa wanatakiwa kwenda kupiga picha maalum za wadhamini wa timu ya taifa, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL).
  Lakini Mwandila amesema wachezaji hao walirudi baada ya saa 8:00 usiku tena baada ya Mratibu wa Yanga SC, Hafidh Saleh kumpigia simu Nyanda kulalamikia kuchelewa kwa wachezaji hao. 
  “Kulikuwa kuna haraka gani ya kuwachukua wachezaji hao jana, kwa nini wasingesubiri tumalize mechi. Lakini mbona wachezaji wengine wote wa timu ya taifa hawakuchukuliwa kutoka Azam, Simba wapo Uturuki na timu za mikoani. Kwa nini ilikuwa Yanga tu,”alihoji Mwandila.
  Mzambia huyo alisema mambo ya aina hiyo huwezi kustaajabu soka ya Tanzania iko chini, kwa sababu badala ya viongozi wa TFF kuzisaidia klabu zifanye vizuri kwenye mashindano zinashiriki kuzididimiza.
  Yanga SC imeendelea kufanya vibaya kwenye mechi zake za Kundi D Kombe la Shirikisho la Afrika, baada ya leo kuchapwa mabao 3-2 na Gor Mahia ya Kenya Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Matokeo haya yanamaanisha Yanga inaendelea kukamata mkia katika kundi D, ikibaki na pointi yake moja iliyovuna kwenye sare ya 0-0 na Rayon Sport ya Rwanda kutokana na kufungwa mechi nyingine tatu, mbili dhidi ya Gor Mahia ukiwemo wa wiki mbili zilizopita waliochapwa 4-0 mjini Nairobi.
  Mechi nyingine ambayo ilikuwa ya kwanza kabisa, Yanga ilichapewa mabao 4-0 na USM Alger mjini Algiers nchini Algeria.
  Yanga wataikaribisha USM Alger Agosti 19 kabla ya kwenda kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na wenyeji, Rayon Sport Agosti 28, mwaka huu mjini Kigali, Rwanda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WADAI TFF IMEWAFUNGISHA KWA GOR MAHIA LEO…ILIONDOA NYOTA SITA KAMBINI JANA MCHANA NA KUWARUDISHA USIKU WA MANANE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top