• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 22, 2018

  SIMBA SC YAMSAJILI MZAMBIA CLETUS CHAMA ALIYECHEZA HADI MISRI…AMESAINI MKATABA WA MIAKA MIWILI LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imeendelea kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao, baada ya kumsajili kiungo mshambuliaji, Mzambia Cletus Chama Chota kutoka Lusaka Dynamos ya kwao kwa mkataba wa miaka miwili.
  Chama ambaye alikuwa Nahodha wa Lusaka Dynamos ametambulishwa leo na Kaimu Rais wa klabu, Salim Abdallah ‘Try Again’ mbele ya kocha mpya, Mbelgiji Patrick J Aussems.
  Pamoja na Dynamos, timu nyingine alizowahi kuchezea Chama mwenye umri wa miaka 27 sasa ni Ittehad ya Misri, ZESCO United FC na Nchanga Rangers FC, zote za kwao pia, Zambia.
  Kiungo mshambuliaji, Mzambia Cletus Chama amesaini mkataba wa miaka miwili Simba SC leo
  Cletus Chama (katikati) akiwa na Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ (kushoto) na kocha mpya, Mbelgiji Patrick J Aussems (kulia.  

  Cletus Chama (katikati) akisaini mkataba huku akishuhudiwa na Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ (kushoto) na kocha mpya, Mbelgiji Patrick J Aussems (kulia)  

  Na usajili huo umefanyika saa chache kabla ya kikosi cha Simba kupanda ndege kwenda Uturuki kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya.
  Chama anakuwa mchezaji mpya wa tatu wa kigeni, baada ya beki Muivory Coast, Serge Wawa Pascal na mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere.
  Hao wanaungana na Waghana, beki Asante Kwasi, kiungo James Kotei na mshambuliaji Nicholas Gyan, Waganda Emmanuel Okwi, Juuko Murshid, Mrundi Laudit Mavugo na Mnyarwanda Haruna Niyonzima.
  Hata hivyo, kuna uwezekano Juuko na Mavugo wakatajwa katika orodha ya wachezaji wanaoachwa baada ya ujio wa Kagere na Wawa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAMSAJILI MZAMBIA CLETUS CHAMA ALIYECHEZA HADI MISRI…AMESAINI MKATABA WA MIAKA MIWILI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top