• HABARI MPYA

    Sunday, July 29, 2018

    YANGA SC YAFUNGA KWA MARA YA KWANZA MAKUNDI AFRIKA IKICHAPWA 3-2 NA GOR MAHIA TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imefanikiwa kufunga mabao kwa mara ya kwanza katika Kundi D Kombe la Shirikisho la Afrika, lakini ikipoteza mechi ya tatu kwa kulambwa 3-2 na Gor Mahia ya Kenya Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Matokeo haya yanamaanisha Yanga inaendelea kukamata mkia katika kundi D, ikibaki na pointi yake moja iliyovuna kwenye sare ya 0-0 na Rayon Sport ya Rwanda kutokana na kufungwa mechi nyingine tatu, mbili dhidi ya Gor Mahia ukiwemo wa wiki mbili zilizopita waliochapwa 4-0 mjini Nairobi.
    Mechi nyingine ambayo ilikuwa ya kwanza kabisa, Yanga ilichapewa mabao 4-0 na USM Alger mjini Algiers nchini Algeria.

    Mfungaji wa bao la pili la Yanga leo, Raphael Daudi akiwatoka wachezaji wa Gor Mahia Uwanja wa Taifa

     Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na marefa kutoka Mauritius Ahmad Imtehaz Heeralall aliyepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Cauvelet Louis Ralph Fabien na Akhtar Nawaz Rossaye, Gor Mahia ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza 2-0.
    K’Ogalo walipata bao lao la kwanza dakika ya kwanza tu, mfungaji George Odhiambo Ogutu aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Mcameroon Youthe Rostand Juhe baada ya mpira wa juu wa Kevin Omondi.
    Yanga SC wakajaribu kutulia kupunguza kasi ya Gor Mahia huku wakisaka bao la kusawazisha, lakini jitihada zao zilidumu hadi dakika ya 40 tu, kabla ya kuwaruhusu wageni kupata kupata bao la pili dakika ya 41 lililofungwa na Mnyarwanda Jacques Tuyisenge kwa shuti la mbali baada ya kuanzishiwa mpira na kiungo Mkenya, Francis Kahata mpira wa adhabu ndogo.
    Katika kipindi hicho, Gor ingeweza kuondoka na mabao zaidi kama ingetumia nafasi zake nyingine dakika ya 18 na 34 wakati Odhiambo alipofumua mashuti yaliyodakwa na kipa wa Yanga, Rostand. 
    Yanga ilikaribia kufunga mara moja tu kipindi hicho baada ya shuti la mpira wa adhabu lililopigwa na beki Juma Abdul kutoka nje sentimita chache kwenye lango la Gor Mahia.
    Kipindi cha pili Yanga SC walikianza vizuri na kufanikiwa kupata bao la kwanza kabisa katika hatua hii ya makundi, mfungaji kiungo Deus Kaseke dakika ya 59 aliyekuwa anacheza mechi yake ya kwanza tangu arejee kutoka Singida United alipodumu kwa msimu mmoja.
    Gor Mahia wakaimarisha uongozi wao kwa bao la tatu lililofungwa na Nahodha Harun Shakava dakika ya 64, kabla ya kiungo Raphael Daudi kuifungia Yanga bao la pili dakika ya 81.
    Yanga wataikaribisha USM Alger Agosti 19 kabla ya kwenda kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na wenyeji, Rayon Sport Agosti 28, mwaka huu mjini Kigali, Rwanda.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Youthe Rostand/Benno Kakolanya dk77, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Pius Buswita, Yussuf Mhilu/Juma Mahadhi dk54, Papy Kabamba Tshishimbi, Matheo Anthony, Raphael Daudi na Deus Kaseke/Ibrahim Ajib dk61.
    Gor Mahia: Boniface Oluoch, Humphrey Mieno, Philemon Otiemo, George Odhiambo/Bernard Ondiek dk90, Haron Shakava, Joash Onyango, Kevin Omondi/Lawrence Juma dk63, Jacques Tuyisenge/Charles Momanyi dk83, Francis Kahata, Samuel Onyango na Godfrey Walusimbi. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAFUNGA KWA MARA YA KWANZA MAKUNDI AFRIKA IKICHAPWA 3-2 NA GOR MAHIA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top