• HABARI MPYA

  Alhamisi, Julai 26, 2018

  RASMI SASA DILUNGA NI MCHEZAJI HALALI WA SIMBA, ANAKWENDA KAMBINI UTURUKI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Mtibwa Sugar ya Morogoro imeridhia kiungo wake Hassan Dilunga kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC baada ya makubaliano ya pande zote.
  Katibu Msaidizi wa Mtibwa Sugar, Abubakar Swabur ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba wamefikia makubaliano na Simba SC na kuanzia sasa Diliunga si mchezaji wao tena anahamia klabu ya Dar es Salaam.
  Baada ya msimu mzuri akiisaidia Mtibwa Sugar kutwaa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) naye kuibuka mchezaji bora wa mashindano, Dilunga anarejea klabu kubwa.
  Miaka mitano iliyopita Simba SC ilijaribu kumsajili Dilunga kutoka Ruvu Shooting, lakini wakazidiwa kete na mahasimu wao, Yanga SC waliokuwa wanatambia fedha za mfadhili na Mwenyekiti wao wa wakati huo, Yussuf Manji.

  Hassan Dilunga sasa ni mchezaji halali wa mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC  

  Hata hivyo, baada ya misimu miwili Dilunga aliondoka Yanga kufuatia kutofautiana na aliyekuwa Katibu wa wakati huo, Jonas Tiboroha na kurejea Ruvu Shooting katika Ligi Daraja la Kwanza hadi kuisaidia kupanda Ligi Kuu, kabla ya kuhamia JKT Ruvu na baadaye Mtibwa.
  Dilunga sasa ataungana na kikosi cha Simba SC kilichoweka kambi katika hoteli ya Reen Park & Resorts mjini Istanbul nchini Uturuki kujiandaa na msimu mpya, kikifanya mazoezi kwenye moja ya viwanja vitano vilivyopo kwenye hoteli hiyo.
  Wachezaji waliopo na Simba SC kambini mjini Istanbul, Kaskazini Mashariki mwa Uturuki ni makipa Deo Munishi ‘Dida’, Aishi Manula, Ally Salim; mabeki ni Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Serge Wawa, Yussuf Mlipili, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Paul Bukaba.
  Viungo ni Haruna Niyonzima, Mohammed Ibrahim ‘Mo’, Rashid Juma, James Kotei, Muzamil Yassin, Jonas Mkude, Cletus Chama na Shiza Kichuya, washambuliaji Meddie Kagere, Marcel Kaheza, Abdul Hamisi, Emmanuel Okwi, Nahodha John Bocco, Adam Salamba na Mohammed Rashid.
  Kiungo Said Ndemla hajasafiri na timu kwa sababu yupo kwenye mipango ya kujiunga na klabu ya AFC Eskilstuna ya Sweden akiwa amemaliza mkataba wake Simba, wakati mshambulaji Mrundi, Laudit Mavugo ameachwa na beki Mganda, Juuko Murshid ameruhusiwa kwenda kutafuta timu nyingine. 
  Makipa Said Mohammed Ndunda na Emmanuel Mseja, beki Ally Shomari, kiungo Jamal Mwambeleko na mshambuliaji Moses Kitandu ambao wote hawajasafiri na timu kwenda Uturuki kwa sababu wanatafutiwa timu za kuchezea kwa mkopo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RASMI SASA DILUNGA NI MCHEZAJI HALALI WA SIMBA, ANAKWENDA KAMBINI UTURUKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top