• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 28, 2018

  KILIMANJARO QUEENS WAREJEA KWA BASI NA KOMBE LAO BAADA YA USHINDI WA JANA

  Na Mwandishi Wetu, KIGALI
  PAMOJA na kufanikiwa kutetea Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa Wanawake, CECAFA Challenge baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Ethiopia Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali, Rwanda jana, lakini timu ya Tanzania Bara inarejea kwa basi.
  Viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakiongozwa na Rais, Wallace Karia, watapanda ndege kurejea Dar es Salaam kifahari, wakati wachezaji waliopigania heshima ya nchi wakisota barabarani kwa zaidi ya Kilomita 1500 kurudi nyumbani na Kombe lao kwa basi.
  Ushindi wa jana uliifanya Kilimanjaro Queens kumaliza na pointi saba sawa na Uganda, baada ya kushinda mechi mbili, sare moja na kufungwa moja lakini wastani wao mzuri wa mabao unawapa taji la pili mfululizo la CECAFA Challenge.

  Ethiopia ilitangulia kwa bao la Meseru Abera dakika ya 29 kabla ya Tanzania kuzinduka kipindi cha pili na kuwafanyia ‘ubaya’ mabinti wa Kihabeshi kwa mabao ya Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ dakika ya 46, Donisia Daniel dakika ya 56, Stumai Abdallah dakika ya 61 na Fatuma Mustafa dakika ya 89.
  Ethiopia imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake sita, wakati Kenya imekuwa ya nne kwa pointi zake nne sawa na wenyeji, Rwanda walioshika mkia.
  Pamoja na kuburuza mkia, lakini Rwanda ndiyo timu pekee iliyowafunga mabingwa Tanzania Bara, 1-0 katika mchezo wa kwanza kabisa.
  Kilimanjaro Queens wakiwa chini ya kocha Bakari Shime, aliyekuwa anasaidiwa na Edna Lema wanafanikiwa kutetea taji walilolibeba mwaka 2016.
  Mwaka 2016 michuano hiyo ilifanyika kwa mtindo wa makundi, baadaye mtoano kuanzia Nusu Fainali wakati mwaka huu mashindano yamechezwa kwa mtindo wa Ligi, na bingwa ameamuliwa kwa pointi nyingi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KILIMANJARO QUEENS WAREJEA KWA BASI NA KOMBE LAO BAADA YA USHINDI WA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top