• HABARI MPYA

    Friday, July 20, 2018

    KILI QUEENS WAKIFURAHIA MAISHA KIGALI BAADA YA KIPIGO CHA RWANDA

    Na Mwandishi Wetu, KIGALI
    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens, Bakari Shime amesema wachezaji wake watapambana kuhakikisha wanashinda mechi ya leo dhidi ya Kenya na kurejesha matumaini ya kutetea ubingwa wa Kombe la Challenge wanaoushikilia.
    Kilimanjaro Queens ilifungwa na Rwanda (She- Amavubi) bao 1-0  wakati Kenya nao walilala kwa idadi hiyo walipocheza na Uganda kwenye mechi zao za kwanza zilizofanyika juzi kwenye Uwanja wa Kigali.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online jana, Shime alisema wanafahamu mahali walipokosea katika mechi ya kwanza na hawahitaji kuona wanarudia makosa waliyofanya katika mchezo uliopita.
    Wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens, kutoka kulia Fatuma Issa 'Fetty Densa,' Fatuma Hatibu 'Foe', Fatuma Issa 'Didier Fetty' na Evelline Sekikubo wakifurahia kwenye bwawa la kuogelea la hoteli ya Hilltop mjini Kigali, Rwanda 

    Shime alisema kuwa wameshawaona wapinzani wao walivyo, na sasa wamejipanga kufanya vizuri ili warejeshe matumaini ya kutetea ubingwa wao.
    "Tutacheza kwa kiwango cha juu kadri ya uwezo, tunahitaji kushinda ili turudi kwenye mashindano, naamini timu yangu kesho (leo) itakuwa tofauti na ilivyokuwa katika mechi dhidi ya Rwanda, tumejipanga kupambana zaidi," alisema Shime.
    Nahodha wa timu hiyo, Asha Rashid alisema kuwa leo watashuka uwanjani wakiwa makini zaidi na kutumia vyema nafasi ambazo watazitengeneza.
    "Tuliumia sana, hatutaki kupoteza tena mchezo, naamini kila mmoja wetu atajituma kuhakikisha tunapata ushindi, nafasi bado tunayo kama tutashinda mechi zetu tatu zilizobakia," alisema mshambuliaji huyo wa timu ya Kilimanjaro Queens na JKT Queens.
    Mechi nyingine itakayochezwa leo ni kati ya Uganda dhidi ya Ethiopia wakati Kilimanjaro Queens itashuka tena dimbani Jumatatu kuwavaa Uganda na itamaliza mechi zake Julai 27 mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Ethiopia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILI QUEENS WAKIFURAHIA MAISHA KIGALI BAADA YA KIPIGO CHA RWANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top