• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 22, 2018

  WACHEZAJI YANGA SC ‘WAPEWA MANENO’ NA KUKUBALI KUREJEA MAZOEZINI KESHO…BIN KLEB ASEMA HATA TATIZO MTU YANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WACHEZAJI wa Yanga wamekubali kuendelea na mazoezi kesho baada ya ahadi nzuri kwenye kikao na uongozi leo makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani mjini Dar es Salaam.
  Wachezaji wa Yanga waligoma kufanya mazoezi baada ya kurejea kutoka Kenya Alhamisi ambako Jumatano walipigwa mabao 4-0 na wenyeji, Gor Mahia katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Moi Kasarani mjini Nairobi – kushinikiza kulipwa malimbikizo ya mishahara yao.
  Na leo viongozi wa Yanga, Hussein Ndama, Mussa Katabaro, Mustafa Ulungo na Hussein Nyika wamekutana na wachezaji na wanashughulikia matatizo yao na muda si mrefu watapatiwa haki zao.
  Na wamekubaliana na wachezaji kwenda kambini mjini Morogoro kesho kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Gor Mahia.

  Kwa mazungumzo hayo, wachezaji wa Yanga wamekubali kurudi mazoezini kesho Jumatatu na yataendelea kufanyika Uwanja wa Chuo cha Maafisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini mjini Dar es Salaam asubuhi kabla ya mchana kwenda Morogoro kuweka kambi.  
  Yanga SC iliendelea kuvurunda Julai 18 ikikamalisha mechi tatu za mzunguko wa kwanza bila ushindi, ikifungwa mbili zote 4-0, ya kwanza dhidi ya MC Alger nchini Algeria Mei 6 na sare ya 0-0 na Rayon Sport mjini Dar es Salaam Mei 16. 
  Yanga wataikaribisha Gor Mahia Julai 29 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano kabla ya kurudiana na USM Alger Agosti 19 na kwenda kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na wenyeji, Rayon Sport Agosti 28.
  Wakati huo huo: Kiongozi wa zamani wa Yanga SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema kwamba hana tatizo na mtu yeyote kati ya viongozi wa klabu na kujiweka kwake kando kwa sasa ni kwa sababu za kiafya na shughuli za biashara zake.
  “Nasikitika sana baadhi ya vyombo vya Habari vinavyoandika kwamba mimi nitarudi Yanga Sanga akiondoka. Mimi bado nipo Yanga, isipokuwa tu si kiongozi. Na nimekataa uongozi kwa sababu za kiafya na pia nimebanwa mno na majukumu ya biashara zangu,” amesema.

  Abdallah Bin Kleb (katikati) enzi zake akiwa kiongozi Yanga. Kulia ni mchezaji Mrisho Ngassa na kushoto kiongozi mwenzake, Seif Ahmed 'Seif Magari' ambaye pia hayupo madarakani kwa sasa

  Bin Kleb alikuwa kiongozi wa Yanga kwa mafanikio mwanzoni hadi katokati ya muongo huu, kabla ya kujiuzulu kwa sababu ya majukumu ya biashara na familia. Pamoja na mara kadhaa kuteuliwa katika Kamati mbalimbali, lakini amekuwa akikataa kwa sababu hizo hizo.
  Lakini Bin Kleb amekuwa akitoa michango yake ya kifedha wakati wote tangu amejiondoa kwenye uongozi mwaka 2016. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WACHEZAJI YANGA SC ‘WAPEWA MANENO’ NA KUKUBALI KUREJEA MAZOEZINI KESHO…BIN KLEB ASEMA HATA TATIZO MTU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top