• HABARI MPYA

  Jumanne, Julai 24, 2018

  UTETEZI WA RAIS WA TFF, WALLACE KARIA JUU YA KUONGEZA WACHEZAJI WA KIGENI LIGI KUU

  "Ndugu zangu waandishi wa habari. Nimewaita leo hapa kuja kuzungumzia suala la wachezaji kumi wa kigeni kucheza katika ligi kuu ya nchi yetu.nimeona nilizungumzie kutokana na maoni mbalimbali yanayotolewa na watu tofauti kuhusu jambo hili.
  Kwanza nianze na utaratibu wetu wa upitishaji wa kanuni, huko nyuma kulikuwa na migogoro mingi juu ya kutoshirikishwa kikamilifu kwa vilabu wakati wa upitishaji kanuni. Ili kuondoa migogoro hiyo TFF iliamua kuwa mchakato wa kanuni mbali na kushirikisha wadau wengine lakini vilabu vipewe uzito katika masuala yanayohusu kanuni za ligi zetu.

  Rais wa TFF, Wallace Karia (kulia) akiwa na Kaimu Makamu wake, Athumani Nyamlani katika mkutano wake na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam

  Hivyo kama kawaida vilabu vya ligi kuu kupitia aliyekuwa mwenyekiti wao wa bodi ya ligi waliitisha kikao 30Juni,2018 katika ukumbi wa mikutano uwanja wa Taifa kuzungumzia masuala kadhaa likiwemo suala la kanuni mpya za Ligi Kuu.
  Baada ya kikao cha Bodi ya Ligi walileta mapendekezo ya kanuni mbalimbali kwa kamati ya Utendaji ya TFF ili yapitishwe, moja ya mapendekezo yao ilikuwa ni mabadiliko ya kanuni ya 57, ambapo walipendekeza ongezeko la wachezaji wa kigeni kutoka saba mpaka wachezaji 10.mapendekezo ya kanuni yalijadiliwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya tff na wakakubaliana na hoja za vilabu vya ligi kuu na kupitisha maombi yao.
  Ndugu waandishi niliona ni vyema kuanza kuwaonyesha utaratibu uliotumika hadi kanuni hii ikapitishwa ili angalau watu waone jinsi tff yangu inavyofanya kazi kwa utawala wa sheria na kuhakikisha vilabu vikiwa ni wadau muhimu wa ligi zetu vinasikilizwa.
  Baada ya majadiliano ya kina kuhusu kanuni na.57, faida za wachezaji wa kigeni ni kama ifuatavyo;

  Kibiashara.
  Ligi kuu ya nchi inapokuwa na wachezaji wa kigeni inavutia uwekezaji mkubwa kwa makampuni mbalimbali kwa sababu ligi inakuwa na mvuto na ushindani mkubwa.
  Lakini pia ligi yetu itakuwa inafuatiliwa kwenye nchi nyingi ambazo wachezaji wanatoka na kuwapa wadhamini wetu fursa pana zaidi kujitangaza.

  Kwenye ukuzaji wa program za vijana.  
  Unapokuwa na ligi yenye mvuto ina maana uwekezaji unakuwa mkubwa na mapato ya ligi yanaongezeka, kwa wenzetu waliondelea faida inayopatikana kwenye ligi ndiyo inasaidia kwenye kuwekeza katika maendeleo ya program za vijana, ndo maana wachezaji wa kigeni wameisaidia ligi kuu ya england kuwa na thamani kubwa, hivyo kupata faida inayowekezwa kwenye program mbalimbali za vijana. Na ushahidi england ndiyo mabingwa wa dunia wa vijana chini ya miaka 17 na chini ya miaka 20. Lakini ligi yao kwa kuwa na wachezaji wengi kutoka nchi mbalimbali kumesaidia uboreshaji wa viwango vya wachezaji wa kiingereza na mafanikio yao ya karibuni ni kufikia nusu fainali ya kombe la dunia.

  Kiufundi.
  Wachezaji wetu watapata nafasi ya kuboresha viwango vyao uchezaji kwa kukutana na wachezaji ambao wana viwango vyenye ubora.
  Lakini pia uwepo wa wachezaji wa kigeni utasaidia vijana wetu kujifuza kuwa mpira ni kazi hivyo kuhakikisha wanatunza viwango vyao.

  Maslahi ya wachezaji wetu.
  Kipindi hiki ambacho wachezaji wa kigeni wamekuwa wanasajiliwa imesaidia pia wachezaji wetu kuboreshewa mishahara.

  Kuhusu Timu za Taifa.
  Maendeleo ya mpira wa miguu yamebadilika sana. Vikosi vya timu za taifa vimekuwa vikitegemea wachezaji wanaocheza kwenye ligi zenye ubora wa juu wakiamini wachezaji wanaocheza ligi hizo wanapata ushindani mkubwa na wanaweza kushindana.
  Nitatoa mifano ya vikosi vya vya timu za taifa vilivyoshiriki mashindano ya kombe la dunia kutoka afrika.
  Misri kwenye kikosi cha kwanza kilichoanza kulikuwa kuna wachezaji wanne tu wanaocheza ligi ya nyumbani na ikizingatiwa ligi ya misri ni miongoni mwa ligi bora tulizonazo afrika.
  Nigeria kwenye kikosi cha kwanza walichokuwa wanaanza kulikuwa hakuna mchezaji hata mmoja anayecheza ligi ya nyumbani.
  Senegal kwenye kikosi chao cha kwanza kilichokuwa kinaanza kilikuwa na mchezaji mmoja tu aliyekuwa anacheza ligi ya nyumbani.
  Tunisia kwenye kikosi cha kwanza walikuwepo wachezaji wanne wanaocheza nyumbani.
  Morocco kwenye kikosi chao cha kwanza hakukuwa na mchezaji hata mmoja wa ndani, na ikumbukwe hawa ndiyo mabingwa wa kombe la chan lakini hata mchezaji mmoja hakuwa na nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza.
  Kwenye kombe la dunia nitoe mfano wa timu mbili za ubelgiji na ufaransa.
  Ufaransa ambao ndiyo mabingwa wachezaji waliokuwa wanaanza kikosi cha kwanza ni wachezaji wawili tu waliokuwa wanapata nafasi ya kuanza.na wote tunajua ubora wa ligi ya ufaransa.
  Ubelgiji kwenye kikosi chao cha kwanza cha Timu ya Taifa kulikuwa hakuna mchezaji hata mmoja aliyekuwa anaanza kwenye kikosi cha kwanza.
  Hii inatupa fundisho hili tuwe na kikosi imara cha Timu ya Taifa Taifa Stars ni vyema tukawekeza kwa wachezaji wetu kupata nafasi ya kucheza kwenye ligi zenye ubora. Hivyo wakati tunaimarisha ligi yetu ni vyema pia vijana wetu wakapata firsa ya kutoka na kucheza ligi za wenzetu zenye ubora wa hali ya juu.
  Sasa nisemee kuhusu takwimu za wachezaji wa kigeni kwa msimu uliopita.
  Tulikuwa na timu za ligi kuu 16 zilizopaswa kusajili wachezaji 480, idadi ya wachezaji wa kigeni waliosajiliwa ni 40 ikiwa ni asilimia 8.3.
  Hivyo wachezaji wazawa ilikuwa ni zaidi ya asilimia 90. Hivyo ikionyesha kwamba bado ligi yetu ina namba ya wachezaji wazawa wa kutosha kwa idadi ya zaidi ya asilimia 90.

  Msimu wa mwaka 2018/2019.
  Kwa msimu huu mpaka tunapoongea wachezaji wa kigeni na vilabu vilivowasajili ni kama ifuatavyo,
  1.Simba-8
  2.Yanga-2
  3.Azam-6
  4.Singida-5
  5.Biashara-4
  6.Stand United-4
  7.Mbeya City-1
  8. KMC FC-2

  Hadi muda huu wachezaji waliombewa wa kigeni ni 32. Ikiwa ni asilimia 5 ya wachezaji watakaosajiliwa.wakati dirisha linafungwa alhamisi 26July,2018 kwa idadi iliyopo tunategemea idadi ya wachezaji wa kigeni itapungua tofauti na msimu uliopita tuliokuwa na asilimia 8 ya wachezaji wa kigeni.
  Na wachezaji wa kigeni waliosajiliwa na vilabu vya ligi kuu lazima watimize masharti ya kikanuni kwa kusajili mchezaji anayecheza timu ya taifa au ligi kuu , au vyote viwili awe mchezaji wa ligi kuu na timu ya taifa.
  Kanuni hii imewekwa ili kuwalinda wachezaji wetu kwa kuwa na wachezaji wenye ubora ambao watasaidia kuboresha viwango vya wachezaji wetu na thamani ya ligi yetu.
  Ndugu zangu waandishi wa habari baada ya kusema haya niseme kama rais wa TFF nimepokea maoni mbalimbali tunaweza kupima sisi wenyewe kama kuna athari kubwa inayotokana na kanuni hii basi tuna nafasi ya kukaa chini na vilabu ili tuifanyie mabadiliko,".
  (Haya ni maelezo ya Rais wa TFF, Wallace Karia katika mkutano wake na Waandishi wa Habari leo Julai 24,2018 mjini Dar es Salaam)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: UTETEZI WA RAIS WA TFF, WALLACE KARIA JUU YA KUONGEZA WACHEZAJI WA KIGENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top