• HABARI MPYA

    Tuesday, July 31, 2018

    AZAM FC YAANZA KUJIFUA VIKALI UGANDA KUJIANDAA NA MSIMU MPYA...WATACHEZA MECHI NNE ZA KUJIPIMA

    Na Mwandishi Wetu, KAMPALA
    MABINGWA wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC wameanza mazoezi ya nguvu katika kambi yao ya mjini Kampala nchini Uganda kujiandaa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Agosti 22, mwaka huu.
    Msafara wa Azam FC uliwasili jana mchana nchini Uganda na kujichimbia katika Hoteli ya Top Five, iliyopo Ntinda mjini Kampala kwa kambi ya wiki mbili itakayohusisha mechi zisizopungua nne za kirafiki kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam Agosti 16 mwaka huu.
    Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi, limeonekana kujipanga kuiandaa vema timu hiyo kutokana na mazoezi makali ya wanayowapa wachezaji hao tangu jana asubuhi.
    Wachezaji wote wamejumuika kwenye programu hiyo, isipokuwa winga Joseph Kimwaga na mshambuliaji Donald Ngoma, wanaofanya programu ya mazoezi mepesi na Nahodha Mkuu Agrey Morris, aliyepewa mapumziko ya siku kadhaa kutokana na kuwa mgonjwa.
    Kocha Mkuu wa Azam FC, Mholanzi Hans van der Pluijm akiwapa mazoezi kwa mifano wachezaji wa timu hiyo mjini Kampala leo asubuhi 

    Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Nahodha Msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi’, alielezea kufurahishwa na mazingira ya kambi kiujumla huku akiwaambia mashabiki wa timu hiyo watajiandaa vema kwa ajili ya kuonyesha ushindani msimu ujao.
    “Kwanza tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufika salama Uganda, tunajiandaa vizuri kwa sababu tunafuata maelekezo ya kocha, programu nzuri, tunakaa Hoteli nzuri kumetulia, ni jambo la kila mchezaji kujiandaa vizuri, kuonyesha jitihada mazoezini mwisho wa siku tuweze kupata matokeo mazuri msimu ujao,” alisema.
    Matarajio makubwa ya Azam FC kwenye ziara hii wanayoifanya kwa mara ya tatu, ni kukiandaa vema kikosi hicho kiufundi na kimwili ili kuweza kukabiliana na ushindani kuelekea msimu ujao 2018-2019 na kutwaa makombe kama ilivyofanya mwezi uliopita ilipotwaa kwa mara ya pili mfululizo michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAANZA KUJIFUA VIKALI UGANDA KUJIANDAA NA MSIMU MPYA...WATACHEZA MECHI NNE ZA KUJIPIMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top