• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 29, 2018

  UVUMILIVU NA UMOJA UTAWAFIKISHA YANGA KANANI

  Na Masau Bwire, PWANI
  KLABU ya Yanga, leo Jumapili, July 29, 2018, kuanzia saa 1.00 jioni, itajitupa katika uwanja wa Taifa, Dar Es salaam kupambana na Gor Mahia ya Kenya. 
  Ni mchezo muhimu sana kwa Yanga, zaidi sana ikihitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri kimsimamo katika mashindano hayo, kwani mpaka sasa Yanga ina point moja tu, inashika mkia katika kundi ililopo. 
  Nafasi bado ipo, kubwa tu kwa Yanga kufanya vizuri,  pengine kufuzu kucheza hatua inayofuata baada ya hii inayoendelea, inawezekana sana tu, msikate tamaa, pambaneni kiume, mafanikio yapo.
  Najua mmepitia magumu mengi, makubwa mno, ya kuchosha,  kudhoofisha na kukatisha tamaa, haya yote yafanyeni ngazi ya kupandia kuelekea mafanikio.

  Yanga SC leo inashuka dimbani mjini Dar es Salaam kumenyana na Gor Mahia ya Kenya

  Kumbukeni ugumu waliokutana nao Wana wa Israel katika safari yao ya kutoka Misri kwenda Kanani, safari ilikuwa ndefu, ngumu, yenye vikwazo vingi, lakini walifika salama baada ya kuvumilia na kuzikabili vilivyo changamoto zilizoibuka safarini.
  Wana Yanga, msichoke, japo safari ni ndefu na ngumu, vumilieni, jipeni moyo, msichoke na kukata tamaa, tianeni moyo, mnyanyueni anayechoka, shirikianeni kwenye shida katika safari hii ndefu na ngumu, mtafika salama kwa mafanikio. 
  Ebu leo jitokezeni kwa wingi, ingieni uwanjani kwa maelfu, elfu yenu, shangilieni kwa nguvu, mshikamane kweli kweli, hakika ninaamini,  kwa kuyafanya hayo, mtafika KANANI salama kwa mafanikio makubwa, wengi, hasa Mahasimu wenu, wataduwaa mmefikaje Kanani, wakati wao wanashangaa mmefikaje, maana waliwadharau, ninyi muda huo mtakuwa mmesahau shida na masumbuko yote,  mtakuwa kwenye raha, mkinywa maziwa na asali, kwa raha zenu, mkitafuna BATA bila Bughudha....
  Umoja ni silaha muhimu na kubwa mno katika kushinda vita dhidi ya adui, unganeni, kuweni wamoja, mtashinda vita, mkianza leo dhidi ya Gor Mahia.
  Yanga Mbele daima, nyuma mwiko. 
  (Mwandishi wa makala hii, Masau Kuliga Bwire ni Ofisa Habari wa klabu ya Ruvu Shooting FC ya Pwani)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: UVUMILIVU NA UMOJA UTAWAFIKISHA YANGA KANANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top