• HABARI MPYA

  Ijumaa, Julai 27, 2018

  KILIMANJARO QUEENS MABINGWA TENA KOMBE LA CHALLENGE, WAIPIGA ETHIOPIA 4-1 MECHI YA MWISHO

  Na Mwandishi Wetu, KIGALI
  TANZANIA Bara imefanikiwa kutetea Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Ethiopia leo Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali, Rwanda.
  Ushindi huo umeifanya Kilimanjaro Queens kumaliza na pointi saba sawa na Uganda, baada ya kushinda mechi mbili, sare moja na kufungwa moja lakini wastani wao mzuri wa mabao unawapa taji la pili mfululizo la CECAFA Challenge. 
  Ethiopia ilitangulia kwa bao la Meseru Abera dakika ya 29 kabla ya Tanzania kuzinduka kipindi cha pili na kuwafanyia ‘ubaya’ mabinti wa Kihabeshi kwa mabao ya Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ dakika ya 46, Donisia Daniel dakika ya 56, Stumai Abdallah dakika ya 61 na Fatuma Mustafa dakika ya 89.

  Ethiopia imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake sita, wakati Kenya iliyoichapa Rwanda 2-0 katika mchezo wa mwisho usiku huu imekuwa ya nne kwa pointi zake nne sawa na wenyeji, Amavubi walioshika mkia.
  Pamoja na kuburuza mkia, lakini Rwanda ndiyo timu pekee iliyowafunga mabingwa Tanzania Bara, 1-0 katika mchezo wa kwanza kabisa.
  Kilimanjaro Queens wakiwa chini ya kocha Bakari Shime, aliyekuwa anasaidiwa na Edna Lema wanafanikiwa kutetea taji walilolibeba mwaka 2016 wakiwafunga, Kenya 2-1 katika fainali.
  Mwaka 2016 michuano hiyo ilifanyika kwa mtindo wa makundi, baadaye mtoano kuanzia Nusu Fainali wakati mwaka huu mashindano yamechezwa kwa mtindo wa Ligi, na bingwa ameamuliwa kwa pointi nyingi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KILIMANJARO QUEENS MABINGWA TENA KOMBE LA CHALLENGE, WAIPIGA ETHIOPIA 4-1 MECHI YA MWISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top