• HABARI MPYA

    Sunday, July 29, 2018

    BMT, TFF WASAIDIE KUWASHINIKIZA VIONGOZI YANGA WAITISHE UCHAGUZI HARAKA

    KWA mara nyingine Yanga SC imejikuta haina viongozi wote wa juu, kufuatia kujiuzulu kwa pia kwa Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga Julai 23, mwaka huu.
    Sanga alitangaza kujiuzulu wadhifa huo katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika hoteli ya Protea (Courtyard), Oysterbay mjini Dar es Salaam, akisema amelazimika kufanya hivyo baada ya kutishiwa maisha kufuatia kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Gor Mahia ya Kenya kwenye mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika wiki mbili zilizopita.
    Sanga amekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga SC tangu Mei mwaka jana kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Mehboob Manji.

    Hiyo ni baada ya Sanga na Manji kuingia madarakani Yanga katika uchaguzi uliofanyika Julai 15, mwaka 2012 na matokeo kutangazwa Alfajiri ya siku iliyofuata ukumbi wa Diamond Jubilee, Upanga mjini Dar es Salaam.
    Sanga aliyepigiwa debe na Manji, alipata kura 1948 dhidi ya 475 za Yono Kevela na 288 za Ayoub Nyenzi katika uchaguzi amabo Abdallah Bin Kleb, Moses Katabaro, Aaron Nyanda na Geroge Manyama walichaguliwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
    Nao hao waliingia madarakani kupitia uchaguzi mdogo, ulioitishwa baada ya viongozi wote wa juu, Mwenyekiti Lloyd Nchunga na Makamu wake, Davis Mosha kujiuzulu pia.
    Baada ya safu hiyo kumaliza muda wake, Juni 12, mwaka 2016 ukafanyika uchaguzi mwingine na wote wawili wakatetea nafasi zao, Manji ambaye hakuwa na mpinzani alipata kura 1,468 kati ya 1,470 na Sanga alipata 1,428 kati ya 1,508 akimshinda Tito Osoro aliyepata kura 80.
    Waliochaguliwa kuwa wajumbe wa kamati ya utendaji, idadi ya kura zikiwa kwenye mabano ni Siza Augustino Lymo (1027), Omary Said Amir (1069), Tobias Lingalangala (889), Salum Mkemi (894), Ayoub Nyenzi (889), Samuel Lukumay (818), Hashim Abdallah (727) na Hussein Nyika (770).
    Hao waliwashinda David Luhago (582), Godfrey Mheluka (430), Ramadhani Kampira (182), Edgar Chibura (72), Mchafu Chakoma (69), George Manyama (249), Bakari Malima 'Jembe Ulaya' (577), Lameck Nyambaya (655), Beda Tindwa (452), Athumani Kihamia (558), Pascal Lizer (178) na Silvester Haule (197).  
    Lakini katika awamu zote mbili, Sanga alionekana kuwa na kazi nyepesi kutokana na nguvu ya Mwenyekiti wake, Manji kiuchumi, utendaji na ushawishi.
    Mambo yalianza kuwa magumu Yanga na kwa Sanga baada ya Manji kujiuzulu Mei mwaka jana baada ya miaka 11 akianza kama mfadhili mwaka 2006.
    Limekuwa pigo kubwa kuondoka kwa Manji Yanga, ambaye alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
    Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
    Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
    Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
    Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.
    Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
    Na ni katika kipindi hicho imeshuhudiwa Manji amewazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
    Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
    Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
    Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
    Kwa sasa klabu inakabiliwa na hali ngumu kiuchumi kiasi cha kuambulia ushindi wa mechi moja kati ya 14 zilizopita, nyingine saba wakifungwa na sita kutoa sare. Na wana Yanga wako tayari Manji arejee kwa sharti lolote kuinusuru klabu.
    Haikuwa ajabu Juni 10, mwaka huu katika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, wanachama wa Yanga SC pamoja na kuunda Kamati ya Kusimamia Timu kwa Wakati huu chini ya Mwenyekiti, Tarimba Abbas, pia waligomea ombi la Mei mwaka jana la Mwenyekiti wao, Manji kujiuzulu na kusema bado wanamtambua kama kiongozi wao mkuu.
    Lakini waliunda Kamati ya watu tisa chini ya Rais wa zamani wa klabu, Tarimba na wanachama wa Yanga Kusimamia Shughuli mbalimbali za klabu hiyo kufuatia kile kinachoonekana kuelemewa kwa uongozi uliopo madarakani sasa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Sanga.
    Mwenyekiti Mteule wa Kamati hiyo ni Tarimba Abbas, Makamu wake, Saidy Meckysadik na Wajumbe wa Kamati hiyo ni Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Lucas Mashauri, Yusuphed Mhandeni, 
    Na hiyo ni kutokana na kupwaya kwa Kamati ya Utendaji kutoka uongozi uliochaguliwa Juni mwaka 2016 imepungua mno baada ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti mwenyewe, Yussuf Manji na Wajumbe wa Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.  
    Waliobaki katika Kamati ya Utendaji pamoja na Sanga ni Wajumbe wanne, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika. Lakini Kamati hiyo ilifarakana na uongozi wa Sanga na Tarimba akatangaza kujiuzulu wiki mbili zilizopita ingawa baadaye wawili hao walikutanishwa kwa suluhu na kutangaza kumaliza tofauti zao.
    Wakati anajiuzulu Sanga alisema anaikabidhi timu kwa Baraza la Wadhamini kwa mujibu wa Katiba, lakini siku moja baadaye Wajumbe waliobaki katika uongozi huo, wakaitisha mkutano kumtangaza Omar Kaaya kuwa Kaimu Katibu Mkuu mpya, anayechukua nafasi ya gwiji wa klabu, Charles Boniface Mkwasa aliyejiuzulu katikati ya mwezi huu.
    Idadi kubwa ya wanachama hawana imani na watu ambao wapo na timu kwa sasa, lakini nao wameendelea kung’ang’ania wakijinasibu wao ndiyo viongozi halali.
    Uzuri hawakatai kwamba klabu inahitaji kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi za vongozi waliojiuzulu na kulingana na agizo la Waziri Mwakyembe katika mkutano wa Juni 10, mwaka huu uitishwe uchaguzi wa kujaza nafasi hizo ndani ya miezi mitatu ni matarajio hilo ndilo linalofuata muda si mrefu, hususan baada ya idadi ya waliojiuzulu kuongezeka.
    Yanga inaelekea mwisho wa matatizo yake baada ya Sanga kujiuzulu, kwani sasa lazima uchaguzi ufanyike hata kama Manji atakubali ombi la wanachama kubatilisha uamuzi wa kujiuzulu, lakini utafanyika uchaguzi kuziba nafasi za Makamu na Wajumbe kadhaa walioondoka.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ndivyo vyombo ambavyo kwa sasa vintegemewa sana na wana Yanga kuhakikisha vinasaidia agizo la Waziri Mwakyembe kutekelezwa kwa viongozi waliopo kuitisha uchaguzi haraka iwezekanavyo.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BMT, TFF WASAIDIE KUWASHINIKIZA VIONGOZI YANGA WAITISHE UCHAGUZI HARAKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top