• HABARI MPYA

    Monday, July 30, 2018

    KCB WASAINI MKATABA MPYA NA TFF KUENDELEA KUDHAMINI LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesaini mkataba mpya na benki ya Biashara ya Kenya (KCB) kuendelea kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa msimu wa 2018/2019 wenye thamani ya Shilingi Milioni 420.
    Rais wa TFF, Wallace Karia amesema kwamba KCB wataendelea kuwa wadhamini wenza wa Ligi Kuu ambayo mdhamini wake mkuu atatajwa baadaye.
    Zoezi la kusaini mkataba huo mpya limefanyika katika hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam asubuhi ya leo katika mkutano na Waandishi wa Habari. 
    Ligi Kuu msimu wa 2018-2019 inatarajiwa kuanza Agosti 22, ikitanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya mabingwa watetezi, Simba SC dhidi ya washindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation (ASFC), Mtibwa Sugar ambao utafanyika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Agosti 18.

    Rais wa TFF, Wallace Karia (kushoto) wakati wa kusaini mkataba mpya leo mjini Dar es Salaam

    Mechi za ufunguzi za Ligi Kuu zitachezwa Agosti 22 kati ya Ruvu Shooting na Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Alliance na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na Coastal Union na Lipuli FC ya Iringa Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. 
    Mechi nyingine ni kati ya Singida United na Biashara United Uwanja wa Namfua, Singida, Kagera Sugar na Mwadui FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba zote Saa 10:00 jioni na Simba SC na Tanzania Prisons Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
    Mahasimu wa jadi, Simba na Yanga watakutana Septemba 30, mwaka huu katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu utakamilishwa Agosti 23 kwa mechi kati ya JKT Ruvu na KMC Saa 8:00 mchana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Stand United na African Lyon Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na Azam FC dhidi ya Mbeya City Saa 1:00 usiku.
    Mtendaji Mku wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura amesema kwamba msimu huu Ligi itaanza Agosti 22, 2018 na kufikia tamati Mei 19, mwakani (2019) ikiwa na jumla ya mechi 380 kutoka 240 msimu uliopita baada ya ongezeko la timu nne kutoka 16 za msimu uliopita.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KCB WASAINI MKATABA MPYA NA TFF KUENDELEA KUDHAMINI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top