• HABARI MPYA

    Sunday, July 29, 2018

    KILIMANJARO QUEENS WAKUTANA NA KATIBU WA WIZARA DODOMA KABLA YA KUENDELEA NA SAFARI KUREJEA DAR

    Na Mwandishi Wetu, DODOMA
    KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Suzan Mlawi leo ameupokea msafara wa timu ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Queens’ makao makuu ya nchi mjini Dodoma ukitokea mjini Kigali, Rwanda ambako juzi walitwaa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.
    Baada ya mapokezi hayo na kuwapa pongezi, msafara wa Kilimanjaro Queens uliowasili Dodoma Alfajiri ukitokea Kigali kwa basi, uliendelea na safari kurejea Dar es Salaam ambako unatarajiwa kuwasili jioni.
    Pamoja na kufanikiwa kutetea Kombe la CECAFA Challenge baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Ethiopia Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali, Rwanda Ijumaa, lakini Kilimanjaro Queens wanarejea nyumbani kwa basi, jambo ambalo limewasikitisha wapenzi wengi wa soka.
    Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Suzan Mlawi akipokea Kombe la CECAFA Challenge kutoka kwa  Nahodha wa Kilimanjaro Queens, Asha Rashid 'Mwalala'

    Wachezaji wa Kilimanjaro Queens wakiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Suzan Mlawi mjini Dodoma leo

    Viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakiongozwa na Rais, Wallace Karia wamepanda ndege kurejea Dar es Salaam kifahari, wakati wachezaji waliopigania heshima ya nchi wakisota barabarani kwa zaidi ya Kilomita 1500 kurudi nyumbani na Kombe lao kwa basi.
    Ushindi wa Ijumaa uliifanya Kilimanjaro Queens kumaliza na pointi saba sawa na Uganda, baada ya kushinda mechi mbili, sare moja na kufungwa moja lakini wastani wao mzuri wa mabao unawapa taji la pili mfululizo la CECAFA Challenge. 
    Ethiopia ilitangulia kwa bao la Meseru Abera dakika ya 29 kabla ya Tanzania kuzinduka kipindi cha pili na kuwafanyia ‘ubaya’ mabinti wa Kihabeshi kwa mabao ya Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ dakika ya 46, Donisia Daniel dakika ya 56, Stumai Abdallah dakika ya 61 na Fatuma Mustafa dakika ya 89.
    Ethiopia imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake sita, wakati Kenya imekuwa ya nne kwa pointi zake nne sawa na wenyeji, Rwanda walioshika mkia.
    Pamoja na kuburuza mkia, lakini Rwanda ndiyo timu pekee iliyowafunga mabingwa Tanzania Bara, 1-0 katika mchezo wa kwanza kabisa.
    Kilimanjaro Queens wakiwa chini ya kocha Bakari Shime, aliyekuwa anasaidiwa na Edna Lema wanafanikiwa kutetea taji walilolibeba mwaka 2016.
    Mwaka 2016 michuano hiyo ilifanyika kwa mtindo wa makundi, baadaye mtoano kuanzia Nusu Fainali wakati mwaka huu mashindano yamechezwa kwa mtindo wa Ligi, na bingwa ameamuliwa kwa pointi nyingi. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILIMANJARO QUEENS WAKUTANA NA KATIBU WA WIZARA DODOMA KABLA YA KUENDELEA NA SAFARI KUREJEA DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top