• HABARI MPYA

    Sunday, July 05, 2015

    AZAM FC WASIKUBALI KUUZIWA MBUZI KWENYE GUNIA

    BAADA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitisha kanuni ya kutumia wachezaji saba wa kigeni katika Ligi Kuu kutoka watano, klabu zimeanza kwenda mbio kusajili wageni zaidi.
    Simba SC imemsaini kwa miaka miwii mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’ wakati na Yanga SC wamesajili Mzimbabwe Donald Ngoma na Mghana Joseph Tetteh Zutah.
    Azam FC imeleta kipa wa zamani wa mabingwa wa England, Chelsea FC, Vincent Atchouailou de Paul Angban aliyewasili juzi usiku Dar es Salaam. 
    Mlinda mlango huyo aliyezaliwa Februari 2, mwaka 1985 mjini Anyama kwa mujibu wa wasifu wake, aliwasili pamoja na wachezaji wengine wawili wa Azam FC raia wa Ivory Coast, beki Serge Wawa Pascal na mshambuliaji KIpre Tchetche.
    Kipa huyo mrefu anayetokea klabu ya Ligi Kuu ya kwao, Ivory Coast, Jeunesse jana asubuhi alikuwepo mazoezini Azam FC katika ufukwe wa Coco Beach, Dar es Salaam.
    Vincent Angban aliwahi kuchezea timu ya vijana ya Chelsea chini ya umri wa mika 21 ingawa alikuwa amevuka umri huo katika harakati za kutafuta kusajiliwa The Blues, lakini pamoja na kuonyesha uwezo Stamford Bridge, haikuwa bahati yake jezi ya bluu.
    Kipa huyo aliibukia katika klabu ya vijana ya Rio Sport d'Anyama kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2005, ambako hata hivyo miaka miwili baadaye aliondoka na kwenda kujiunga na Sawe Sports msimu wa 2006/2007.
    Mwaka 2007, Angban akajiunga na ASEC Mimosas ambako alikuwa kipa wa kwanza hadi mwanzoni mwa msimu wa 2009 alipoumia na nafasi yake kuchukuliwa na Daniel Yeboah. 
    Yeboah akawavutia zaidi makocha wa timu hiyo kwa ubora wake wa kuokoa michomo na akaendelea kudaka hata Angban alipopona.
    Baada ya kumaliza Mkataba wake ASEC, Angban akarejea Jeunesse na baadaye akaenda London kudakia U21 ya Chelsea.
    Amewahi kudakia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Ivory Coast katika michuano ya Afrika nchini Benin mwaka 2005 na aliiwakilisha pia nchi yake katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2008.
    Amedakia pia timu ya taifa ya wakubwa ya Ivory Coast ‘Tembo’ katika michuano ya CHAN ikiwemo ile ya mwaka 2009 na ndiye aliyesimama langoni katika mechi na Tanzania, Taifa Stars ikishinda 1-0 bao pekee la Mrisho Ngassa.   
    Azam FC inataka kumchukua kipa huyo kwa lengo la kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya michuano ya Afrika- na kama inavyojulikana timu hiyo ya bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake mwakani itacheza Kombe la Shirikisho. 
    Akisaini Azam FC, kipa huyo atakwenda kugombea namba na makipa wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Aishi Manula na Mwadini Ali.
    Kabla ya kuanza kwa ligi ya Bara hapo Agosti 22 mwaka huu, Azam pia imeshaanza maandalizi kwa ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) ambayo yatafanyika nchini kuanzia wiki ijayo.
    Usajili wa kipa huyo ukikamilika, Azam itakuwa na wachezaji wanne kutoka Ivory Coast, wengine ni Serge Wawa Pascal na pacha, Kipre Herman Tcheche na Kipre Michael Balou.
    Awali wakati nasoma wasifu wa kipa huyo kuona alifika hadi Chelsea, akawekwa kwenye kikosi cha vijana kujaribiwa, niliamini atakuwa kipa bora.
    Lakini hata klabu alizochezea Ivory Coast ni kubwa- pia amechezea timu ya taifa ya nchi yake na alicheza michuano ya CHAN ya kwanza ambayo wao walikuwa wenyeji.
    Kweli. Amedakia Ivory Coast hadi kwenye Fainali za vijana chini ya umri wa miaka 20 nchini Benin mwaka 2005 na aliiwakilisha pia nchi yake katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2008.
    Lakini jana nimemuona mtu ambaye kama alijitoa mchezoni kwa muda- ama alipumzika soka kabisa, au alikuwa majeruhi wa muda mrefu na hajafanya mazoezi.
    Anaweza kuwa kipa mzuri, lakini Azam FC inapaswa kujiridhisha kwanza juu ya hilo, ili isikubali kurudia makosa iliyowahi kuyafanya siku za nyuma.
    Sote tunakumbukua kuhusu washambuliaji Mamadou Kone kutoka Ivory Coast pia na Ismail Diarra kutoka Mali waliotua Azam FC miaka ya karibuni na kupatiwa mikataba minono, lakini wakashindwa kuthibitisha uwezo.
    Walikuja na wasifu mzuri ambao uliwashawishi Azam FC wakatoa maelfu ya dola za Kimarekani yenye thamani ya mamilioni ya shilingi kuwasajili, lakini mwisho wa siku wakalipwa tena ili kuvunjiwa mikataba.
    Ndiyo, Azam klabu tajiri lakini sidhani kama inafurahia hasara hizi na ama itakuwa tayari kuendelea kubeba hasara za aina hii, au kuvumilia uzembe wa aina yoyote unaosababisha hasara za aina hiyo.
    Maana yake sasa, wakati umefika uongozi wa Azam FC na benchi la Ufundi uwe makini mno kabla ya kusajili mchezaji yeyote ambaye hawamjui.
    Mchezaji yeyote mpya ambaye hawamjui, afanyiwe majaribio ya kina na apewe mechi ngumu acheze uwezo wake uonekane kama utakuwa na tija katika timu au la- Azam FC wasikubali kuuziwa mbuzi kwenye gunia tena. Ramadhani Karim. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC WASIKUBALI KUUZIWA MBUZI KWENYE GUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top