• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 29, 2015

  UBUNGE WAMTOKEA PUANI MZEE YUSSUF, 'WAPINZANI' WAPASUA KIOO GARI LAKE

  KATIKA hali inayoonyesha kuwa vita vya kisiasa vimekolea hadi kuvuka mpaka, gari la mfalme wa taarab, Mzee Yussuf anayewania ubunge huko Zanzibar limevunjwa kioo.
  Mzee Yussuf mkurugenzi wa Jahazi Modern Taarab aliyetangaza nia ya kusaka ubunge katika jimbo la Fuoni kupitia tiketi ya CCM, amekuwa mtu tishio miongoni mwa watangaza nia wenzake na sasa inaelekea vimeanza vita vya kumpunguza kasi.
  Alfajiri ya leo, gari Toyota Noah analotumia kwenye kampeni zake, limekutwa limevunjwa kioo na kupenyezwa ujumbe unaosema: “Nyie si mnaweza, haya fanyeni sasa”.
  Mzee Yussuf ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE kwamba ni mapema mno kusema lolote, ingawa anaamini kabisa kuwa hiyo ni vita ya kisiasa.
  “Siwezi kusema lolote kwa sasa hivi, lakini naamini hii ni vita ya kisiasa kutoka kwa wapinzani wangu, tumeripoti polisi, kwahiyo nisingependa kuongea mengi kwa muda huu,” alisema Mzee Yussuf.
  Tangu kampeni za ndani ya chama zianze kuelekea kura za maoni, Mzee Yussuf ameonekana wazi kuwa ana ‘mtaji’ mkubwa wa wapiga kura.
  Mzee Yussuf ndiye mgombea mwenye mvuto na ushawishi mkubwa zaidi kwa wana CCM wa Fuoni na hiki kilichotokea alfajiri ya leo kinatafsiriwa kama njia za kinyemela za kumpunguza kasi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: UBUNGE WAMTOKEA PUANI MZEE YUSSUF, 'WAPINZANI' WAPASUA KIOO GARI LAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top