• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 25, 2015

  SIMBA SC YAMREJESHA MWINYI KAZIMOTO, ASAINI MIAKA MIWILI

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa klabu ya Al Markhiya ya Qatar, Mwinyi Kazimoto Mwitula (pichani) amerejea klabu yake ya zamani, Simba SC.
  Habari ambazo hazijathibitishwa na upande wowote, zinasema kwamba Kazimoto amesaini Mkataba wa miaka miwili kama mchezaji huru baada ya kumaliza Mkataba wake Qatar.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe hakupatikana kwenye simu, wakati Kaimu Katibu Mkuu, Collins Frisch alikuwa ‘anaitazama’ tu simu yake ilipokuwa inaita.
  Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva hupokea simu ‘anapojisikia’ na Kazimoto hakupatikana kabisa kwenye simu yake alipotafutwa kuzungumzia habari hizo.  
  Kama amesajiliwa, Kazimoto atakuwa mkongwe wa pili kurejeshwa kikosini Simba SC, baada ya Mussa Hassan Mgosi aliyesaini mwezi uliopita kutoka Mtibwa Sugar.
  Pamoja na wakongwe hao, Wekundu wa Msimbazi pia wamewasajili Peter Mwalyanzi kutoka Mbeya City, Mohamed Fakhi kutoka JKT Ruvu, Samih Haji Nuhu kutoka Azam FC na Emmanuel Mtambuka aliyekuwa huru.
  Mei mwaka huu, Simba SC ilimsajili pia kipa Mohammed Abrahman Mohammed wa JKU ya Zanzibar, lakini klabu yake ikataka fedha nyingi za uhamisho na klabu hiyo ikaamua kuachana naye.
  Kazimoto aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1988 mjini Dodoma, alijiunga na Simba SC mwaka 2011 akitokea JKT Ruvu aliyoanza kuichezea mwaka 2007 baada ya kupandishwa kutoka timu ya vijana.
  Mapema mwaka 2013, Kazimoto aliuzwa timu ya Daraja la Pili Qatar, Al Markhiya ambako baada ya miaka miwili anarejea nyumbani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAMREJESHA MWINYI KAZIMOTO, ASAINI MIAKA MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top