• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 22, 2015

  HUU NI USAJILI MAKINI KWELI WALIOFANYA YANGA SC, AU?

  BAADA ya Yanga SC kutolewa katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu, makocha wa timu hiyo, Mholanzi Hans van der Pluijm na mzalendo Charles Boniface Mkwasa walisema msimu ujao wataboresha kikosi ili waweze kufika mbali.
  Makocha hao walisema kwamba wamegundua aina ya wachezaji walionao kikosini, wengi wao ni kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, lakini ili wafanye vizuri katika michuano ya Afrika wanahitaji watu wengine.
  Bahati nzuri mwishoni mwa msimu, Yanga SC wakafanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, maana yake msimu ujao, watacheza Ligi ya Mabingwa.
  Tayari Yanga SC imekamilisha usajili wa wachezaji wa kigeni baada ya kuongeza wawili, beki Mghana Joseph Tetteh Zutah na mshambuliaji Donald Ngoma kutoka Zimbabwe.
  Hao wanaungana na viungo Mkongo Mbuyu Twite anayeweza kucheza kama beki pia, Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Mbrazil Andrey Coutinho na washambuliaji Kpah Sherman wa Liberia na Mrundi Amisi Tambwe.
  Katika usajili wa wachezaji wa  nyumbani, Yanga SC imewasajili makipa Benedictor Tinocco kutoka Kagera Sugar, Mudathir Khamis, beki Mwinyi Hajji Mngwali wote kutoka KMKM, mawinga Deus Kaseke kutoka Mbeya City, Godfrey Mwashiuya kutoka Kemondo na mshambuliaji Malimi Busungu kutoka Mgambo JKT.         
  Kutoka kikosi cha msimu uliopita, Yanga SC imewapoteza Mrisho Ngassa aliyehamia Free State Stars ya Afrika Kusini, Jerry Tegete, Danny Mrwanda, Nizar Khalfan walioachwa wakati Hassan Dilunga ametolewa kwa mkopo Stand United.
  Baada ya msimu uliopita, Yanga SC ilionekana kabisa inahitaji kusajili beki japo mmoja wa kati na kiungo wa ulinzi wa kiwango cha kimataifa.
  Mbuyu Twite anatumika kama kiungo mkabaji, lakini bado unaweza kuona yule ni beki tu kutokana na staili yake ya uchezaji. 
  Hawezi kutelezea mipira miguuni mwa wapinzani na hawezi kupandisha timu kwa kasi inayotakiwa na si mtoaji wa pasi nzuri za kuanzisha mashambulizi- ni mzuiaji mzuri ambaye anapotumika kama kiungo wa chini, anaimarisha ukuta tu.
  Salum Telela ni kiungo mzuri pale mbele, anachezesha timu vizuri, anatoa pasi nzuri na ni mwepesi- labda tu anatakiwa apunguze mambo mengi ya kuwapigisha mayowe mashabiki.
  Haruna Niyonzima sina tatizo naye, kama anacheza akiwa amezungukwa japo na viungo wawili wakabaji, atakuwa huru na kusaidia sana timu kushambulia.
  Ukiondoa Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, mabeki wengine wa kati Yanga SC ni chipukizi Pato Ngonyani na Rajab Zahir ambao bado hawajaaminiwa.
  Nina matumaini sana na Ngonyani kama muda si mrefu anaweza kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza Yanga SC kutokana na bidii yake. Zahir ni mchezaji mzuri, lakini sioni jitihada zake pamoja na kipaji alichojaaliwa.
  Lakini bado Yanga SC inahitaji beki mmoja wa kati imara atakayeingia kutoa upinzani kwa Yondan na Cannavaro, ili waongeze bidii nao.
  Inavyoonekana kwa sasa, Cannavaro na Yondan wote ni kama wameridhika- kwa sababu ni wao tu kuanzia Yanga SC hadi timu ya taifa.
  Tena inawezekana ‘wamevimba vichwa’ zaidi baada ya kutokuwepo kwenye timu ya taifa kwenye Kombe la COSAFA Juni mwaka huu na waliochukua nafasi zao wakachemsha.
  Maana yake, kama wapo waliokuwa wanadhani mabeki hao hawafai, sasa watafuta ‘usemi wao’ na kujenga imani kwamba kwa sasa Tanzania mabeki wa kati ni Yondan na Cannavaro tu.
  Katika safu ya ushambuliaji Yanga SC imejiimarisha, ingawa tu sina uhakika kama imesajili aina ya wachezaji waliotakiwa na makocha- kwa maana ya watakaomudu mikiki ya michuano ya Afrika, au la.
  Ni kweli Yanga SC imekosa beki wa kulia hapa nyumbani hadi kuleta Mghana Zuttah? Labda.
  Lakini Yanga SC walipaswa kuzitumia vizuri nafasi za wachezaji wa kigeni kwa kusajili aina ya wachezaji ambao kweli kwa sasa hawapatikani kwa urahisi Tanzania mfano viungo na washambuliaji.
  Kweli makocha wanaweza kutoa mapendekezo na hawapaswi kuingiliwa, lakini wanaweza kushauriwa.
  Yanga SC walipaswa kushauriana na kocha wao, Pluijm ambaye ndiye amemleta Zuttah juu ya matumizi mazuri ya nafasi za wachezaji wa kigeni.
  Juma Abdul anacheza vizuri beki ya kulia. Mbuyu Twite pia anaweza kucheza nafasi hiyo. Bado tena ameongezwa Zuttah kwa ajili ya beki kulia, huu ni usajili makini kweli Yanga SC? 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HUU NI USAJILI MAKINI KWELI WALIOFANYA YANGA SC, AU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top