• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 20, 2015

  OLUNGA ‘TISHA MBAYA’ KOMBE LA KAGAME, APIGA MBILI GOR MAHIA YAITANDIKA KMKM 3-1

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI chipukizi wa Kenya, Michael Olunga amefunga mabao mawili Gor Mahia ikiibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya KMKM ya Zanzibar katika mchezo wa Kundi A Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
  Olunga sasa anafikisha mabao matatu na kupiga kasi kwenye mbio za kiatu cha dhahabu cha mshindano ya Kagame 2015 Dar es Salaam.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo, Gor Mahia walipata bao la kwanza dakika ya tano, mfungaji mshambuliaji wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Medie Kagere.
  Lilikuwa bao ambalo lilitokana na kazi nzuri ya Olunga aliyefunga pia Gor Mahia ikiilaza Yanga SC 2-1 katika mchezo wa kwanza wa kundi hilo.
  Michael Olunga ameendelea kutisha kwa mabao Kombe la Kagame 2015

  Timu ya kocha Ally Bushiri, KMKM ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 12 kupitia kwa Mateo Anthony aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Fakhi Mwalimu.
  Timu hizo zilikwenda kupumzika zikiwa zimefungana bao 1-1 na kipindi cha pili, ndipo Gor Mahia wakaongeza mabao mawili zaidi yote yakifungwa na Olunga dakika ya 69 akimalizia pasi ya Mnayarwanda Karim Nizigiyimana na dakika ya 80 kwa shuti kali akimalizia mpira wa uliorushwa na Enock Agwanda.
  Gor inayofundishwa na Mscotland, Frank Nuttal sasa inajiweka katika nafasi nzuri ya kwenda Robo Fainali, baada ya kufikisha pointi sita, ikifuatiwa na KMKM yenye pointi tatu, Khartoum ya Sudan pointi, ambayo katika mchezo wa kwanza imeifunga 5-0 Telecom ya Djibouti, ambayo sasa inashika mkia katika kundi hilo.
  Mabao ya Al Khartoum inayofundishwa na Mghana, Kwesi Appiah yamefungwa na Salah Bilal dakika ya 22, Ousmail Baba dakika ya 67, Wagdi Awad Abdallah dakika ya 78, Murwan Salih Abdallah mawili dakika ya 82 na 89.
  Michuano hiyo inaendelea kesho kwa michezo mitatu, Shandy ya Sudan na LLB AFC ya Burundi, Hegaan ya Somalia na APR ya Rwanda na Malaika ya Sudan Kusini dhidi ya Azam FC ya Tanzania.
  Keshokutwa Khartoum itamenyana na KMKM, KCCA ya Uganda na Adama City ya Ethiopia na Telecom dhidi ya Yanga SC.    
  Kikosi cha KMKM leo kilikuwa: Nassor Abdullah, Khamis Ali, Tizzo Charles, Pandu Haji, Said Idrissa, Mussa Said, Mateo Anthony, Juma Mbwana, Fakhi Mwalim/Iddi Kambi dk73, Ibrahim Khamis na Nassor Ali/Haji Simba dk67. 
  Gor Mahia: Boniface Oluoch, Musa Mohammed, Sibomana Abouba, Harun Shakava, Karim Nizigiyimana, Ali Hassan, Aucho Khalid/George Odhiambo dk85, Godfrey Walusimbi/Enock Agwanda dk65, Ronald Omino/Erick Ochieng dk57, Kagere Medie na Michael Olunga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: OLUNGA ‘TISHA MBAYA’ KOMBE LA KAGAME, APIGA MBILI GOR MAHIA YAITANDIKA KMKM 3-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top