• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 20, 2015

  AYA 15 ZA SAID MDOE: NILISEMA DIAMOND HAZUILIKI, YAMETIMIA

  WIKI chache zilizopita niliandika kuwa kujaribu kumporomosha Diamond ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mkono na sasa hilo linazidi kujidhihirisha baada ya msanii huyo kutwaa tuzo ya kimataifa kupitia MTV Africa.
  Katika tuzo hizo zilizotolewa huko nchini Afrika Kusini kupitia ukumbi wa International Convention Centre ulioko mjini Durban, Diamond akashinda kipengele cha mtumbuizaji bora (Best Live) wa mwaka akiwatupa Big Nuz, Mi Casa wa Afrika Kusini, Flavour wa Nigeria na Toofan wa Togo. 
  Namna ukumbi ulivyolipuka baada ya jina la Diamond kutajwa, ni kielelezo tosha kuwa msanii huyu tayari si wa kwetu tena, si wa kibongo bongo tena, bali ni msanii wa Afrika nzima.

  Watanzania inabidi tubadilike sasa na kumuunga mkono Diamond kwa moyo mmoja, hii ni hatua ya nyingine ya yeye kukwea vidato na tusipokuwa makini basi huko mbele ya safari atatajwa kama Diamond kutoka Afrika na si Diamond kutoka Tanzania – yale yale ya kuambiwa mlima Kilimanjaro uko Kenya.
  Kwa faida ya wale ambao hawakubahatika kusoma kile nilichokuwa nimekiandika katika makala hiyo ya Diamond, naomba nichukue fursa hii kurudia baadhi ya aya zilizochukua uzito mkubwa.
  Kuanzia “Nenda Kamwambie”, “Mbalaga” hadi “Nana”, Diamond hajawahi kushuka, kila ngoma yake mpya ni zaidi ya jana, bei zake za show zinapanda maradufu na sasa sehemu pekee inayostahili kwa maonyesho yake kwa hapa nchini ni kwenye viwanja vya mpira na maeneo mengine kama hayo – enzi za kupiga kwenye kumbi za kuingiza watu 700 zimepita.
  Diamond wa leo ni wa kimataifa, kazi zake zinatambulika kimataifa, anashirikiana na wanamuziki wa kimataifa, anatesa kwenye media za kimataifa.
  Diamond wa leo ni pesa, kila atakachofanya ni pesa, akijitosa kwenye filamu ni pesa, akiamua kuandika kitabu cha maisha yake ni pesa, akitumia jina lake kwenye biashara ya mavazi au bidhaa zozote ni pesa.
  Nini tunachopaswa kukifanya kwa Diamond? Hakuna kingine zaidi ya kumuunga mkono na kumpa heshima inayostahili …kuna nchi kibao zilizoendelea ambazo kila kukicha zinajaribu kuwalinda na kuwakuza ‘masupastaa’ wao wa fani mbali mbali wakiamini hao ni mabalozi wao wazuri popote pale duniani.
  Diamond hakubahatisha kufika hapo alipo bali ni kutokana na jitihada zake, uwezo wake, kipaji chake pamoja na nidhamu hali ya juu.
  Diamond sio mtu wa kupuuza kazi, sio mtu wa kupuuza vyombo vya habari, Diamond anajua namna ya kuwasiliana na dunia – ukitazama mashabiki wake wanamfuata kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na Instagram, utabaki ukiamini kuwa huyo si msanii wa kuporomoka leo au kesho, bado yupo sana kwenye ‘game’.
  Diamond ni aina ya wasanii wanaojifunza mengi kutoka kwa wasanii walipata mafanikio makubwa na kisha wakaporomoka na kubakia kuwa ‘pangu pakavu’ – hawana mbele wala nyuma.
  Wakati Diamond anapenya kwenye tuzo kibao za kimataifa ni vizuri tukamuunga mkono badala ya kumchafua na kumfanyia fitna zisizo na maana, kwa sasa Diamond amefikia hatua ambayo kama utamchukia utapata vidonda vya tumbo bure.
  Ipo tabia moja ya kibinaadamu ambayo inabidi ikemewe sana, nayo ni ile hali ya mtu aliye juu kuchukiwa, kwamba ili mwingine apande ni lazima kumshusha aliye juu na ili kumpandisha mwingine basi ni lazima atengeneze bifu na aliye juu - huu ni ujinga.
  Kila mfalme na zama zake, najua zama za Diamond nazo zitapita, lakini isiwe kwa fitna za kitoto, kufanya hivyo ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mikono – jamaa kishatusua, yuko matawi mengine.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AYA 15 ZA SAID MDOE: NILISEMA DIAMOND HAZUILIKI, YAMETIMIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top