• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 25, 2015

  KIPA WA CHELSEA ATUA SIMBA SC BAADA YA ‘KUDUNDA’ AZAM FC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIPA wa zamani wa mabingwa wa England, Chelsea FC, Vincent Atchouailou de Paul Angban anatarajiwa kwenda Zanzibar leo kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam.
  Raia hiyo wa Ivory Coast anakwenda Simba SC baada ya kufeli majaribio Azam FC, alikotua mapema mwezi huu kujaribu bahati yake, lakini hakumvutia kocha Muingereza Stewart Hall.
  Kaimu Katibu Mkuu wa Simba SC, Collins Frisch ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE leo kwamba Angban ataangaliwa kwa pamoja na Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Muigereza Dylan Kerr na kocha wa makipa, Abdul Salum Idd kwa wiki moja kabla ya kutoa mapendekezo yao.
  Vincent Agban (kulia) akiwa na mchezaji mwenzake kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche wakati alipokuwa majaribio Azam FC 

  Mlinda mlango huyo aliyezaliwa Februari 2, mwaka 1985 mjini Anyama, amekuja Tanzania akitokea klabu ya Ligi Kuu ya kwao, Ivory Coast, Jeunesse.
  Vincent Angban aliwahi kuchezea timu ya vijana ya Chelsea chini ya umri wa mika 21 ingawa alikuwa amevuka umri huo katika harakati za kutafuta kusajiliwa The Blues, lakini pamoja na kuonyesha uwezo Stamford Bridge, haikuwa bahati yake jezi ya bluu.
  Kipa huyo aliibukia katika klabu ya vijana ya Rio Sport d'Anyama kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2005, ambako hata hivyo miaka miwili baadaye aliondoka na kwenda kujiunga na Sawe Sports msimu wa 2006/2007.
  Mwaka 2007, Angban akajiunga na ASEC Mimosas ambako alikuwa kipa wa kwanza hadi mwanzoni mwa msimu wa 2009 alipoumia na nafasi yake kuchukuliwa na Daniel Yeboah. 
  Yeboah akawavutia zaidi makocha wa timu hiyo kwa ubora wake wa kuokoa michomo na akaendelea kudaka hata Angban alipopona.
  Baada ya kumaliza Mkataba wake ASEC, Angban akarejea Jeunesse na baadaye akaenda London kudakia U21 ya Chelsea.
  Amewahi kudakia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Ivory Coast katika michuano ya Afrika nchini Benin mwaka 2005 na aliiwakilisha pia nchi yake katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2008.
  Amedakia pia timu ya taifa ya wakubwa ya Ivory Coast ‘Tembo’ katika michuano ya CHAN ikiwemo ile ya mwaka 2009 na ndiye aliyesimama langoni katika mechi na Tanzania, Taifa Stars ikishinda 1-0 bao pekee la Mrisho Ngassa.   
  Kwa sasa Simba SC ina makipa watatu, kati yao mmoja tu mzoefu, Ivo Mapunda- wengine ni chipukizi Peter Manyika na Dennis Richard ealipandishwa kutoka timu ya vijana msimu uliopita.
  Mei mwaka huu, Simba SC ilimsajili kipa Mohammed Abrahman Mohammed wa JKU ya Zanzibar, lakini klabu yake ikataka fedha nyingi za uhamisho na klabu hiyo ikaamua kuachana naye.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIPA WA CHELSEA ATUA SIMBA SC BAADA YA ‘KUDUNDA’ AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top