• HABARI MPYA

  Jumanne, Julai 21, 2015

  AIRTEL YAKABIDHI JEZI TIMU 17 TAYARI KWA RISING STAR 2015

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel leo imekabidhi jezi kwa timu za wasichana na wavulana za U-17 zinazoshiriki michuano ya Airtel Rising Stars ambayo inatarajiwa
  kuanza katika ngazi ya mkoa Ijumaa, Julai 24.
  Mkoa wa Dar es Salam unajumuisha mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke huku timu nyingine zikitoka mikoa ya Morogoro, Mbeya, Arusha na Mwanza. Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya soka la Vijana ya TFF
  Ayoub Nyenzi alisema kwamba maandalizi yote kwa ajili ya michuano hiyo ngazi za mikoa yamekamilika.

  Mwenyekiti kamati ya soka la vijana katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),Ayubu Njenza (kushoto) akimkabidhi vifaa vya michezo katibu wa chama cha mpira wa miguu  Wilaya ya Kinondoni,Isaac Mazwile kwaajili ya mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya  Airtel Rising Stars, inayoanza tarehe 24 Julai mkoani Mbeya. katikati ni Afisa Uhusiano Airtel,Jane Matinde. Makabidhiano hayo yalifanyika leo jijini Dar-es-Salaam.

  “Ni matarajio yetu kuwa tutashuhudia mechi zilizojaa ushindani na mvuto na vilevile ningependa kuona mamlaka zinazohusika na usimamizi wa michuano hiyo ngazi ya mkoa zikichagua wachezaji bora ambao wataunda timu za kombaini za mikoa tayari kwa kushiriki fainali hizo
  ngazi ya taifa zitazofanyika jijini Dar es Salaam baadaye mwezi Septemba”,alisema.
  Mkoa wa Mbeya utakuwa wa kwanza kuzindua mashindano yake Julai 24, ikifuatiwa na mkoa wa Dar es Salaam Julai 27, Morogoro Agusti 1 na Arusha Agusti 9, huku Mwanza  wakitarajia kufanya uzinduzi wao mnamo Agusti 15. Wageni rasmi katika hafla za uzinduzi wa mikoa wanatarajiwa
  kuwa wakuu wa mikoa husika.
  Mikoa yote shiriki inatarajiwa kuwa na timu za wavulana na wasichana isipokuwa mkoa wa Arusha ambao unatoa timu ya wasichana pekee na Morogoro inayoshirikisha wavulana tu. Huu ni mwaka wa tano mfululizo ambao michuano hii imekuwa ikifanyika nchini, huku ikichangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa vipaji vyenye manufaa kwa Taifa.
  Ofisa Uhusiano wa Airtel Tanzania Jane Matinde, ameelezea nia ya dhati ya kampuni yake kuendelea kudhamini programu za vijana huku akiomba sapoti kutoka kwa TFF, Wizara inayoshughulikia masuala ya michezo pamoja na wadau wengine wa mchezo wa soka.
  Alisema Airtel Rising Stars mwaka huu inaenda bega kwa bega na kampeni mpya ya ‘It’s Now’ huku nahodha wa Ivory Coast ambaye pia ni kiungo wa Manchester City Yaya Toure akiongoza kampeni hiyo. 
  Kampeni hii inalenga kulea na kukuza vipaji barani Afrika kupitia nyanja mbalimbali kama vile michezo, mtindo wa maisha na mziki lakini vilevile kuwapa mbinu zitazaowawezesha kupata ufumbuzi wa masuala ya
  kiteknolojia na kuona fursa zinazowazunguka.
  Airtel Rising Stars ni program ambayo ipo bara zima la Afrika maalum kwa ajili kuwapa vijana fursa ya kuonesha vipaji vyao na kuwarahisishia makocha kupata vijana ambao watawaendeleza vipaji vyao kwa manufaa ya baadaye.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AIRTEL YAKABIDHI JEZI TIMU 17 TAYARI KWA RISING STAR 2015 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top