• HABARI MPYA

    Wednesday, July 29, 2015

    HAKI ITENDEKE, APATIKANE MSHINDI HALALI YANGA NA AZAM LEO TAIFA

    OFISI zitafungwa mapema. Shughuli mbalimbali Dar es Salaam leo zitasimama mapema na watu watamiminika kwa wingi Uwanja wa Taifa.
    Hakuna kingine huko zaidi ya mchezo wa Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame utakaozikutanisha timu mbili kutoka Manispaa tofauti Jijini.
    Ni Yanga SC ya Jangwani, Kariakoo, Manispaa ya Ilala dhidi ya Azam FC yenye maskani yake Chamazi, Mbade, Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.
    Hizo ni timu mbili ambazo kwa miaka mitatu mfululizo zimekuwa zikipokezana taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Kwa lugha nyingine, hao ndiyo wapinzani katika soka ya Tanzania kwa sasa- Simba SC wanabaki kuwa watani wa jadi tu wa Yanga.
    Yanga SC ilichukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwaka juzi, ikapokonywa na Azam FC mwaka jana, lakini mwaka huu wana Jangwani wamerejesha taji lao.
    Na ni matarajio hata msimu mpya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu zitaendelea kuwa za Yanga na Azam FC- ingawa Simba SC wamepania kufufua makali. 
    Kwa mantiki hiyo, mchezo wa leo ni mkubwa- unaweza kusema ni fainali iliyokuja mapema, kwani hautarajiwi tena mchezo mwingine wa kuvutia mashabiki uwanjani kuliko huu wa leo.
    Labda Yanga SC wasonge mbele, mashabiki wataendelea kumiminika kwa wingi Taifa, ingawa si kwa matarajio ya kiwango cha watu watakaoibuka leo.
    Leo inakuwa mara ya pili, Yanga SC na Azam FC kukutana katika Kombe la Kagame, baada ya mwaka 2012 kukutana katika fainali pale pale Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.
    Julai 28, mwaka 2012 katika mchezo uliochezeshwa na refa Thierry Nkurunziza wa Burundi, Yanga SC walishindi 2-0 katika fainali ya Kagame, mabao ya Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliyehamia Simba SC dakika ya 44 na Said Bahanunzi ‘Spider Man’ aliyehamia Polisi Moro dakika ya 90 na ushei.
    Yanga SC ina mashabiki wengi, lakini Azam FC wanatarajiwa kupewa sapoti na mashabiki wa Simba leo Taifa.
    Wapo wanaoamini eti mashabiki wa Simba SC wataishangilia Yanga leo- kwa sababu wanaamini Azam FC imewapora mchezaji wao, Ramadhani Singano ‘Messi’ kwa ‘ujanja ujanja’. 
    Hakuna hakika juu ya hilo, kitu ‘haramu’ zaidi kwa Simba SC ni Yanga. Na kitu haramu zaidi kwa Yanga ni Simba SC. Unatarajia Simba waishangilie Yanga leo iifunge Azam FC, na watani wao hao katika kusherehekea ushindi wao watamtambia nani?
    Wa kutambiwa ni Simba SC tu hapo na si jambo jepesi leo Yanga kupata shangwe za mahasimu wao. Mwendo unatarajiwa kuwa ule ule. Kwenye kivuli dhidi ya picha ya Yanga, Simba watapigia kura giza.
    Wakati hali halisi ikiwa ni hiyo kuelekea mchezo huo, wasiwasi umeibuka kwamba huenda Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) likawaagiza marefa waibebe Yanga SC kwa sababu ikitolewa mashindano yatakuwa kama ‘yamekwisha’.
    Azam FC haina mashabiki na timu nyingine zote zilizosalia katika hatua hii ni za nje, hivyo CECAFA na waandaaji Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hawatapata fedha tena za viingilio.
    Kwanza sitaki kuamini hilo, kwa sababu CECAFA na TFF bodi zote zinaundwa na viongozi makini, wenye kuheshimu sheria 17 za soka na kaulimbiu ya soka ya kiungwana.
    Mashindano haya bahati nzuri sana yanaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni kubwa, SuperSport ambayo mechi ya leo itatazamwa nchi nyingi duniani.
    Chochote kitakachofanywa na marefa kitaonekana dunia nzima na hiyo siyo tu itawafedhehesha marefa, bali hata CECAFA na TFF wataonekana ‘hawana maana’ pamoja na mashindano yao.
    Tunafahamu changamoto kubwa inayowakabili CECAFA katika uandaaji wa mashindano haya, ukosefu wa fedha kiasi kwamba imejikuta inategemea zaidi fedha za mapato ya milangoni, lakini bado hiyo haiwezi kuhalalisha upindishwaji wa sheria za mchezo.
    Tulishuhudia fainali ya michuano hiyo miaka miwili iliyopita, ikikutanisha wageni watupu mwaka 2013 nchini Sudan, Vital'O ya Burundi ilipoifunga 2–0 APR ya Rwanda katika fainali.
    Tunatarajia na mwaka huu pia kigezo kitakuwa sheria 17 za mchezo na kila mechi atapatikana mshindi halali bila kutengeneza mazingira ya timu fulani kufika fainali ili eti mapato yawe makubwa.
    CECAFA wanaweza kumaliza matatizo yao yao ya kifedha kwa kutafuta wadhamini zaidi, lakini si kuvuruga michezo. Ndiyo maana leo ninasema, haki itendeke na mshindi halali apatikane Yanga na Azam Taifa. Siku njema, mchezo mwema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAKI ITENDEKE, APATIKANE MSHINDI HALALI YANGA NA AZAM LEO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top