• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 25, 2015

  AZAM FC WAFANYA MAUAJI KAGAME, WAWAKUNG’UTA WAHABESHI 5-0 TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imefuzu kwa asilimia 100 Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya kushinda mechi yake ya tatu na ya mwisho ya Kundi C leo dhidi ya Adama City ya Ethiopia.
  Azam FC imeibuka na ushindi wa mabao 5-0 katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam- mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche akifunga mawili, mengine Farid Mussa, Mudathir Yahya na Aggrey Morris.
  Dakika 45 za kwanza zilimalizika Azam FC wakiwa mbele kwa mabao 3-0, Kipre Tchetche akianza dakika za sita akimalizia krosi ya Ame Ali ‘Zungu’ na 18 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Erasto Nyoni.
  Mfungaji wa mabao mawili ya Azam FC, Kipre Tchetche akipongezwa na Erasto Nyoni baada ya kufunga bao la pili 

  Faulo hiyo ilitokana na Kipre Tchetche mwenyewe kuangushwa na beki wa Adama City, Wendosen Milkesa nje kidogo ya boksi upande wa kulia.
  Erasto Nyoni akamsetia Farid Mussa kufunga la tatu dakika ya 31 baada ya kutia krosi mairidadi ya chini chini iliyounganishwa kwa guu la kushoto na kinda huyo aliyekuwa pembezoni mwa lango la Adama kushoto.
  Kipindi cha kwanza, Adama ilimpoteza mchezaji wake, Eshettu Menna aliyetolewa kwa kadi nyekundu na refa Issa Kagabo wa Rwanda baada ya kumkwatua kwa nyuma Farid Mussa dakika ya 20.
  Kipindi cha pili kilipoanza tu, Mudathir Yahya akaifungia Azam FC bao la nne akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi Ame Ali ‘Zungu’ dakika ya 46.
  Na dakika ya 69 Moges Tadese akaonyeshwa kadi ya pili ya njano na kuwa nyekundu, baada ya kuushika kwa makusudi mpira uliopigwa na Mudathir Yahya na kusababisha penalti pia.
  Kipre Tchetche akimtoka beki wa Adama City, Wendosen Milkesa
  Beki wa Adama City, Wendosen Milkesa akijaribu kumzuia Kipre Tchetche wa Azam FC
  Kipre Tchetche alikosa bao la wazi mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kumpiga tobo kipa wa Adam City, Yacob Fiseha lakini mpira ukatoka nje sentimita chache
  Erasto Nyoni akimtoka Nahodha wa Adama City, Suleman Mohamed   Beki mzoefu wa kimataifa wa Tanzania, Aggrey Morris Ambroce akaenda kuifungia Azam FC bao la tano kwa penalti dakika ya 71.
  Kwa matokeo hayo, Azam FC inamaliza kileleni mwa Kundi C kwa pointi zake tisa ikifuatiwa na KCCA yenye pointi sita ambazo zote zinakwenda Robo Fainali, wakati Adama imemaliza bila pointi na inarejea nyumbani, huku Malakia ya Sudan Kusini iliyomaliza na pointi tatu inaweza kufuzu kama mshindi wa tatu bora.  
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Abdallah Kheri, Serge Wawa/Said Mourad dk46, Aggrey Morris/Gardiel Miachel, Mudathir Yahya, Hamid Mao, Jean Baptiste Mugiraneza Ame Ali, Kipre Tchetche/Didier Kavumbangu dk60 na Farid Mussa.
  Adama City; Yacob Fiseha, Suleman Mohamed, 
  Wendosen Milkesa, Moges Tadese, Eshetu  Menna, Biruk Kelbero, Desalegn Debesh/Wendimeneh Zerihum dk40, Erkyi Hun Tesfaye, Temesigen Gitsadik/Biniyam Ayele dk46, Takele Elemayehu na Yonatan Kebede/Henok Gemtesa dk75.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC WAFANYA MAUAJI KAGAME, WAWAKUNG’UTA WAHABESHI 5-0 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top