• HABARI MPYA

  Alhamisi, Julai 30, 2015

  YANGA SC ‘WAIENDEA’ MBEYA AZAM FC, YAPANIA KULIPA KISASI NGAO YA JAMII AGOSTI 22 TAIFA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  WACHEZAJI wa Yanga SC wamepewa mapumziko hadi Jumatatu watakapoanza mazoezi tena mjini Dar es Salaam, kabla ya kwenda kuweka kambi Mbeya kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii Agosti 22 na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa ujumla.
  Yanga SC jana iliaga michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame jana baada ya kupigwa na Azam FC kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, shujaa wa Azam FC alikuwa ni kipa Aishi Salum Manula aliyepangua penalti ya beki mpya wa kushoto wa Yanga SC, Mwinyi Hajji Mngwali.
  Kikosi cha Yanga SC kilichofungwa na Azam FC jana

  Aggrey Morris akaenda kufunga penalti ya mwisho ya Azam FC na kuzima kabisa matarumbeta na shangwe za Yanga SC Uwanja wa Taifa.
  Penalti nyingine za Azam FC zilifungwa na Kipre Herman Tchetche, Serge Wawa Pascal wote raia wa Ivory Coast, John Bocco na Himid Mao, wakati za Yanga SC zilifungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela na Godfrey Mwashiuya.  
  Na akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE leo, Katibu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha amesema kwamba wachezaji wamepewa mapumziko hadi Jumatatu.
  Dk. Tiboroha amesema kwamba timu itaondoka Jumamosi ya wiki ijayo, Agosti 8 kwenda Mbeya kuweka kambi itakayohusisha mechi tatu za kirafiki dhidi ya timu kutoka Zambia na Malawi.  
  “Tutarejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa Ngao dhidi yetu na Azam FC Agosti 22, baada ya hapo tutarudi kambini sasa kwa maandalizi ya Ligi Kuu ambayo itaanza Septemba mapema,”amesema Dk. Tiboroha.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC ‘WAIENDEA’ MBEYA AZAM FC, YAPANIA KULIPA KISASI NGAO YA JAMII AGOSTI 22 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top