• HABARI MPYA

    Tuesday, July 21, 2015

    MFARANSA LIEWIG ASAINI MIAKA MIWILI KUFUNDISHA STAND UNITED

    Liewig kushoto alipotangazwa Stand United jana
    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MFARANSA Patrick Liewig amesaini Mkataba wa miaka miwili kufundisha klabu ya Stand United ya Shinyanga, inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
    Liewig alitangazwa rasmi jana Dar es Salaam na leo anasafiri hadi Shinyanga kwenda kuanza kazi ya kuiandaa timu kwa ajili ya Ligi Kuu inayoanza Septemba.  
    Stand imeridhishwa na falsafa ya ufundishaji ya Mfaransa huyo baada ya kumuona akifanya kazi Simba SC miaka miwili iliyopita, hivyo kuamua kumchukua ahamishie mafanikio yake Shinyanga.
    Liewig ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
    Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
    Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990:  alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
    Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
    Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
    Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
    Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia.
    Januari mwaka 2013 alitua Simba SC ambako alifanya kazi hadi mwishoni mwa msimu alipoondoka kwa sababu ya matatizo ya uongozi wa klabu hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MFARANSA LIEWIG ASAINI MIAKA MIWILI KUFUNDISHA STAND UNITED Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top