• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 26, 2015

  MBUYU TWITE AFIKISHA MECHI 100 YANGA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIUNGO mwenye uwezo wa kucheza nafasi za ulinzi pia, Mbuyu Twite (pichani) leo ametimiza mechi 100 tangu amejiunga na Yanga SC Agosti mwaka 2012 akitokea APR ya Rwanda.
  Twite amecheza kwa dakika zote 90 leo, Yanga ikiilaza 1-0 Khartoum N ya Sudan katika mchezo wa mwisho wa Kundi A Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
  Na pamoja na kucheza kama beki na kiungo wa ulinzi wakati mwingine, lakini Mbuyu Twite ameweza kuifungia Yanga SC mabao matatu katika mechi hizo 100.
  Mbuyu Twite ni mchezaji ambaye Yanga SC ilitumia ‘umafia’ kumbadili njia kuelekea Jangwani badala ya Msimbazi mwaka 2012.
  Baada ya Twite kung’ara na APR katika Kombe la Kagame mwaka 2012, michuano ambayo Yanga SC iliibuka bingwa, Simba SC ilianza mazungumzo naye Dar es Salaam na baadaye aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Ismail Aden Rage akasafiri hadi Kigali kwenda kumalizana naye.
  Na Rage akatokea kwenye picha akiwa anamsainisha Twite, akisema tayari ameingia naye Mkataba tayari kuitumikia SImba SC.
  Mbuyu Twite amekuwa na mchango mkubwa kwa Yanga SC kufika Robo Fainali Kombe la Kagame

  Lakini Twite baadaye akawageuka Simba SC licha ya kuwa tayari amechukua fedha, dola za Kimarekani 32,000 (Sh. Milioni 70) na kuibuka akiwa na kigogo wa Yanga SC, Abdallah Bin Kleb amesaini Jangwani.
  Ukafanyika usanii kwa kumtoa mchezaji huyo APR na kumpeleka FC Lupopo ya DRC, ikielezwa alikuwa anacheza timu ya Rwanda kwa mkopo.
  Lupopo wakamuidhinisha Twite Yanga SC na Simba SC waliokuwa wanajaribu kumuhamisha kutoka Rwanda wakagonga ukuta. Hata hivyo, baadaye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Uenyekiti wa Wakili Alex Mgongolwa ikaamuru Yanga kuilipa Simba SC fedha alizochukua mchezaji huyo dola 32,000 na fidia dola 3,000 kama gharama za usafiri na malazi za Rage Kigali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MBUYU TWITE AFIKISHA MECHI 100 YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top