• HABARI MPYA

    Friday, July 31, 2015

    NGASSA AICHAMBUA YANGA SC, ASEMA HAINA NAMBA 10 NA KILA MCHEZAJI ANATAKA KUFUNGA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa amesema Yanga SC kwa sasa ina matatizo mawili makubwa ya kutatua haraka kabla ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanza.
    Ngassa aliyeondoka Yanga SC Mei mwaka huu kuhamia Free State Stars ya Afrika Kusini, amesema Yanga SC haina mchezaji wa kucheza nafasi ya namba 10 na pia wachezaji wote wa mbele wanataka kufunga.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE jana Dar es Salaam, Ngassa alisema kwamba Yanga SC ina wachezaji wa aina moja tu ambao wote wanaweza kucheza kama namba 9.
    www.binzubeiry.co.tz
    Mrisho Ngassa amerejea Afrika Kusini baada ya kupata kibali cha kuishi na kufanya kazi nchini humo

    “Yanga SC inakosa namba 10. Mchezaji wa kupenya penya pale ndani, Malimi Busungu anaweza kutumika namna hiyo, lakini mechi na Azam alicheleweshwa kuingia uwanjani,”alisema Ngassa.
    Lakini pia mchezaji huyo wa zamani wa Yanga SC amesema kwamba kuna tatizo lingine katika safu ya ushambuliaji la Yanga, kila mchezaji anataka kufunga matokeo yake watu hawatengenezeani nafasi.
    “Kila mtu anataka kufunga yeye, sasa hawatengenezeani nafasi. Ndiyo matokeo yake mnashambulia sana mabao hakuna. Lazima Yanga SC wabadilike,”ameongeza Ngassa.  
    Ngassa alikuwepo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi wakati Yanga SC ikitolewa kwa penalti 5-3 na Azam FC katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
    Na makocha Mholanzi, Hans van der Pluijm na mzalendo, Charles Boniface Mkwasa waliwaanzisha kwa pamoja Mrundi Amisi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma, huku Busungu akianzia benchi.
    Ngassa alikuja mara moja nchini juzi kuchukua kibali cha kuishi na kufanya kazi Afrika Kusini Ubalozi wa nchi hiyo mjini na ameondoka jana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGASSA AICHAMBUA YANGA SC, ASEMA HAINA NAMBA 10 NA KILA MCHEZAJI ANATAKA KUFUNGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top