• HABARI MPYA

  Ijumaa, Julai 24, 2015

  SIMBA SC YAMRUDISHA KIONGERA KCB KWA MKOPO

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imemrudisha mshambuliaji wake, Paul Kiongera (pichani kulia) aendelee kucheza kwa mkopo KCB ya Kenya kwa miezi sita mingine.
  Kaimu Katibu Mkuu wa Simba SC, Collins Frisch ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, wamefikia makubalino na Kiongera aendelee kucheza kwa mkopo KCB.
  “Unajua Kiongera bado hajapona sawa sawa goti lake, sasa tumeona aendelee kubaki KCB kwa mkopo hadi atakapopona vizuri, tutamrejesha kundini,”amesema.
  Simba SC ilimsajili Kiongera msimu uliopita kwa Mkataba wa miaka miwili, lakini akaumia mapema tu na kulazimika kuwa nje msimu mzima.
  Hata hivyo, mchezaji huyo aliyekwenda kufanyiwa upasuaji India, alipopona alijiunga na KCB kwa mkopo na msimu huu Simba SC ikaangalia uwezekano wa kumrudisha kikosini.
  Hata hivyo, baada ya kufanyiwa vipimo mwezi uliopita, ikabainika goti lake bado halijapona sawa sawa na ndiyo maana anarejeshwa KCB akaendelee kucheza kwa mkopo.
  Paul Kiongera aliwahi kuichezea Simba SC mechi tano tu na kuifungia mabao mawili, kabla ya kuumia.
  Simba SC sasa inaweza kumsajili mchezaji mwingine wa kigeni badala ya Kiongera kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu, aungane na Waganda Juuko Murushid, Hamisi Kiiza, Simon Sserunkuma, pamoja na wachezaji wengine wawili kutoka Burundi.
  Kwa ujumla, Simba SC ina nafasi mbili za kusajili wachezaji wa kigeni baada ya Waganda hao na Warundi hao na kwa sasa Kamati ya Usajili ya Wekundu wa Msimbazi, chini ya Mwenyekiti wake, Zacharia Hans Poppe iko ‘mawindoni’. 
  Inaelezwa katika nafasi hizo mbili, Simba SC inataka kusajili kipa na mshambuliaji mmoja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAMRUDISHA KIONGERA KCB KWA MKOPO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top