• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 29, 2015

  AZAM FC WAIMALIZA YANGA SC KWA MATUTA KAGAME

  Nahodha wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor' akimuinua beki Aggrey Morris baada ya kufunga penalti ya mwisho na kuiwezesha timu yao kutinga Nusu Fainali
  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imefanikiwa ‘kuangusha mbuyu’ na kusonga Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kufuatia ushindi wa penalty 5-3 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, shujaa wa Azam FC alikuwa ni kipa Aishi Salum Manula aliyepangua penalti ya beki mpya wa kushoto wa Yanga SC, Mwinyi Hajji Mngwali.
  Aggrey Morris akaenda kufunga penalti ya mwisho ya Azam FC na kuzima kabisa matarumbeta na shangwe za Yanga SC Uwanja wa Taifa.
  Penalti nyingine za Azam FC zilifungwa na Kipre Herman Tchetche, Serge Wawa Pascal wote raia wa Ivory Coast, John Bocco na Himid Mao, wakati za Yanga SC zilifungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela na Godfrey Mwashiuya.  
  Ndani ya dakika 90, Azam ndio walikuwa wa kwanza kufanya mashambulizi katika lango la wapinzani wao katika dakika ya kwanza, lakini mshambuliaji wake, John Bocco, alichelewa kuunganisha krosi ya Shomary Kapombe.
  Beki wa Yanga SC, Juma Abdul akigombea mpira dhidi ya kiungo wa Azam FC, Farid Mussa (kulia)
  Kikosi cha Yanga SC leo
  Kikosi cha Azam FC leo

  Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub 'Cannavaro' akiulinda mpira dhidi ya Nahodha wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor' ili kipa wake, Ally Mustafa 'Barthez' audake
  Mshambuliaji wa Yanga SC, Mzimbabwe Donald Ngoma akimiliki mpira mbele ya beki wa Azam FC, Kheri Abdallah

  Azam itajilaumu kukosa bao la wazi katika dakika ya 35 baada ya shuti la kwanza la Kipre Tchetche kupanguliwa na kipa wa Yanga SC, Ally Mustafa ‘Barthez’ na baadaye Shomary Kapombe akajaribu kumalizia, lakini akapaisha juu.
  Dakika ya tisa kipa wa Yanga, Ally Mustapha ' Barthez' alidaka mpira wa 'tik tak' uliopigwa na Frank Domayo na kuwakosesha wenyeji hao wa Chamazi nafasi nyingine ya kufunga.
  Dakika ya 20 Yanga nayo ilipoteza nafasi ya kufunga ikiwa ni tofauti ya sekunde chache, beki wa Azam kutoka Ivory Coast, Pascal Serge Wawa kutoa kwa kichwa krosi ya Godfrey Mwashiuya ambayo ilikuwa inaelekea langoni mwa Azam.
  Kipre Tchetche alipiga pembeni akiwa jirani na lango la Yanga na kupoteza krosi safi aliyopigiwa na Said Mourad katika dakika ya 52.
  Dakika ya 69, Yanga SC ilipata pigo baada ya beki wake wa kulia, Juma Abdul kuumia na kutoka nafasi yake ikichukuliwa na Mghana, Joseph Tetteh Zuttah. 
  Kwa ujumla kipindi cha pili timu zote zilicheza kwa tahadhari zaidi kana kwamba zilihitaji kwenda kuumalizia mchezo huo katika matuta.
  Azam FC sasa itamenyana na KCCA ya Uganda katika Nusu ya pili Ijumaa, baada ya Khartoum N na Gor Mahia kupambana katika Nusu Fainali ya kwanza.
  Utamu ni kwamba, Nusu Fainali zote zitakuwa marudio ya mechi za makundi, kwanza Azam FC iliifunga 1-0 KCCA katika mechi ya Kundi C na Khartoum N ilitoka sare ya 1-1 na Gor Mahia katika mchezo wa Kundi A.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Agrey Morris, Abdallah Kheri/Said Mourad dk46, Paschal Wawa, Jean Mugiraneza, Himid Mao, Frank Domayo/Ame Ally dk46, Farid Mussa, John Bocco na Kipre Tchetche. 
  Yanga SC: Ally Mustafa ‘Barthez’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Abdul/Joseph Zuttah dk69, Godfrey Mwashiuya, Donald Ngoma, Kevin Yondani, Mbuyu Twite, Deus Kaseke/Salum Telela dk61, Amisi Tambwe, Haruna Niyonzima/Malimi Busungu dk80 na Hajji Mwinyi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC WAIMALIZA YANGA SC KWA MATUTA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top