• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 20, 2015

  WAMBURA ATAKA ‘KUMNG’OA’ AZZAN KINONDONI, RWAMBOW APIGA HATUA RUFIJI, MAJURA ATAKA KUIREJESHA CCM KAWE

  Jamal Rwambow anawania Rufiji
  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WIMBI la wanamichezo na wasanii kuwania ngazi za kisiasa nchini, limeendelea kushika kasi, baada ya wengine kuchukua fomu mwishoni mwa wiki.
  Katibu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Richard Wambura amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Kinondoni.
  Kwa sasa, Mbunge wa Kinondoni ni Idd Mohammed Azzan, Meneja wa zamani wa Simba SC. Wambura pia amewahi kuwa kiongozi wa SImba SC. 
  Naye Mjumbe wa Baraza la Michezo la Tanzania Bara (BMT), Jamal Mandenda Rwambow amerejesha fomu kuwania Ubunge wa Jimbo la Rufiji kupitia CCM.
  Akizungumza jijini jana, Rwambow ambaye ni mdau mkubwa wa michezo alisema kuwa sababu kubwa ya kuomba kuwatumikia wakazi wa jimbo la Rufiji ni kuleta maendeleo ya haraka katika kila sekta.
  Alisema kuwa mbali ya sekta ya michezo, pia amepania kuwakwamua wakaji wa jimbo hilo katika hali ya umaskini waliyokuwa nayo hasa kwa kutumia utajiri wa rasilimali za jimbo hilo ikiwemo bonde la kilimo la mto Rufiji.
  Alifafanua kuwa pamoja na kuweka nia ya kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM, pia ameweka vipaumbele kadhaa ambavyo ndivuo vitawafanya wakazi wa jimbo hilo kupata maendeleo ya kina na si vinginevyo.
  Michael Richard Wambura anawania Kinondoni, ambako yuko Simba mwenzake, Iddi Mohammed Azzan

  “Kwenye michezo nitasaidia timu na kuinua vipaji na kuviendeleza na kufikia hatua ya juu kabisa, jimbo la Rufiji lina wachezaji wengi wa mpira wa miguu, mpira wa kikapu, netiboli na michezo mingine, hata mabondia wapo katika jimbo hilo, hakuna mtu aliyeweza kuwatoa hapo walipo na kufikia kiwango cha kitaifa na kimataifa, kazi hiyo sasa itakuwa ya kwangu mimi,” alisema Rwambow.
  Alisema kuwa aliwajengea uzio wa uwanja wa mpira wa miguu, hatua ambayo iliwawezesha wachezaji kuanza kufaidi matunda ya uchezaji wao baada ya kuanza kupata fedha kidogo kutokana na jasho lao.
  Kuhusiana na sekta nyingine, Rwambow alisema kuwa nyenzo kuu ni kutafuta mitaji, kuweka mipango na kuitekeleza, kufanya kazi kama timu moja, kuyafanya mambo ya maendeleo kwa haraka zaidi na kutambua watendaji bora na kuwakemea wazembe.
  “Nitahakikisha tunafanyakazi pamoja kwa vitendo na siyo kusema tu, hii itakuwa katika sekta zote ambazo ni muhimu kwa binadamu,” alisema.
  Aidha, Mwandishi nguli wa habari za michezo nchini, Abdallah Idrisa Majura naye ameomba ridhaa ya CCM kugombea jimbo la Kawe, ambalo kwa sasa linashikiliwa na Halima Mdee wa Chadema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WAMBURA ATAKA ‘KUMNG’OA’ AZZAN KINONDONI, RWAMBOW APIGA HATUA RUFIJI, MAJURA ATAKA KUIREJESHA CCM KAWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top