• HABARI MPYA

  Alhamisi, Julai 30, 2015

  NGASSA APATA KIBALI CHA KAZI SAUZI NA KUWAAMBIA YANGA; “MLIKOSEA KUMUWEKA BENCHI MSUVA”

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  HATIMAYE kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa amepata kibali cha kuishi na kufanya kazi Afrika Kusini, lakini amesema Yanga SC ilikosea jana kutomchezesha Simon Msuva.
  Ngassa alikuwepo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana wakati Yanga SC ikitolewa kwa penalti 5-3 na Azam FC katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
  Na makocha Mholanzi, Hans van der Pluijm na mzalendo, Charles Boniface Mkwasa hawakumtumia kabisa Mchezaji Bora na Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simon Msuva, aliyeshuhudia mchezo wote akiwa benchi.
  Ngassa aliyewasili jana mchana kuja kuchukua kibali cha kuishi na kufanya kazi Afrika Kusini Ubalozi wa nchi hiyo mjini hapa amesema; “Yanga SC wamekosea kutompanga Msuva,”.
  Mrisho Ngassa (kushoto) na Simon Msuva (kulia) enzi zao wakicheza pamoja Yanga SC 

  Mchezaji huyo mpya wa Free State Stars ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini amesema kwamba Msuva ni mchezaji mwenye kasi na uzoefu, ambaye kama angechezeshwa jana, angeisaidia Yanga.
  “Sijui kwa sababu gani hakucheza, kama alikuwa mgonjwa sawa, lakini alikuwa mzima na wakamuacha benchi tu, basi walikosea,”alisema Ngassa ambaye anaondoka jioni ya leo kurejea Bethelehem yalipo makao makuu ya FS.
  Ngassa amesema kweli Yanga imesajili wachezaji wapya wenye kasi, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya, lakini wote hao kuna vitu wanazidiwa na Msuva, haswa uzoefu.
  “Mwashiuya mzuri, lakini anahitaji muda zaidi ili kujifunza kutokana na makosa yake na kupata uzoefu. Kaseke pia mzuri, si mfungaji sana kama Msuva na ndiyo anaanza kukusanya uzoefu,”amesema mume wa Radhia ‘Nish’.
  Lakini kwa ujumla, Ngassa akamwagia sifa kiungo wa Azam FC, Himid Mao Mkami, kwamba alifanya kazi nzuri ya kutibua mipango ya Yanga uwanjani jana.
  “Himid yeye jana alikuwa mtu wa kuharibu tu, na yule Mugiraneza (Jean Baptiste) alikuwa anasaidia vizuri ulinzi. Na Azam, kama Yanga walikuwa wanatumia mawinga kushambulia. Lakini nilivutiwa sana na Farid Mussa. Peke yake angekuwa mpishi wa mabao matatu kama nafasi alizotengeneza zingetumiwa vizuri,”amesema Ngassa.
  Pamoja na hayo, Ngassa amesema kwamba ushindi wa Azam FC jana haumaanishi Yanga SC ni mbovu, bali ilizidiwa maarifa ya kimchezo na bahati haikuwa yao.
  “Yanga SC wajipange tu, waangalie walikosea wapi wafanye marekebisho, baada ya hapo waje kulipa kisasi kwenye mechi ya Ngao ya Jamii (watakutana tena na Azam). Huo ndiyo mpira,”amesema Ngassa.        
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NGASSA APATA KIBALI CHA KAZI SAUZI NA KUWAAMBIA YANGA; “MLIKOSEA KUMUWEKA BENCHI MSUVA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top