• HABARI MPYA

  Jumanne, Julai 28, 2015

  GOR MAHIA YAICHAPA 2-1 MALAKIA, KUKUTANA NA KHARTOUM N TENA NUSU FAINALI IJUMAA

  Godfrey Walusimbi akipongezwa na mchezaji mwenzake, Michael Olunga baada ya kuifungia Gor Mahia mabao yote katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Malakia ya Sudan Kusini Robo Fainali ya Kombe la Kagame jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

  MATOKEO NA RATIBA KOMBE LA KAGAME 

  ROBO FAINALI
  Julai 28, 2015
  APR (Rwana) 0-4 Khartoum N (Sudan)
  Gor Mahia (Kenya) 2-1 Malakia (Sudan Kusini) 
  Julai 29, 2015
  Al Shandy (Sudan) Vs KCCA (Uganda) (Saa 7:45 mchana)
  Azam FC Vs Yanga SC (zote Tanzania) (Saa 10:15 jioni) 
  NUSU FAINALI
  Julai 31, 2015
  Khartoum Vs Gor Mahia (Saa 8:00 mchana)
  Al Shandy/KCCA Vs Azam/Yanga (Saa 10:00 jioni)
  Agosti 2, 2015 
  MSHINDI WA TATU Saa 8:00 mchana
  FAINALI Saa 10:00 jioni
  GOR Mahia ya Kenya itamenyana na Khartoum N ya Sudan katika Nusu Fainali ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati Ijumaa wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Hiyo inafuatia Gor Mahia inayofundishwa na Mscotland, Frank Nutal kuifunga mabao 2-1 Malakia ya Sudan Kusini katika Robo Fainali ya pili jioni hii Uwanja wa Taifa, Jijini.
  Shujaa wa Gor Mahia leo alikuwa mchezaji wa kimataifa wa Uganda, Godfrey Walusimbi aliyefunga mabao yote hayo kipindi cha kwanza dakika za tatu na 28, yote kwa kazi nzuri ya Michael Olunga.
  Bao pekee la Malakia lilifungwa na Thomas Jacob dakika ya 64 na baada ya hapo, Gor Mahia wakaanza kucheza kwa kujihami zaidi kuhofia kuruhusu bao la kusawazisha.
  Robo Fainali ya kwanza, Khartoum N, washindi hao wa tatu wa Kundi A, nyuma ya Yanga SC na Gor Mahia, waliifunga APR ya Rwanda mabao 4-0 Uwanja wa Taifa.
  Mabao ya Khartoum N inayofundishwa kocha Mghana, Kwesi Appiah yalifungwa na Atif Khali dakika ya 10, Amin Ibrahim dakika ya 19 na 36 na Salah Eldin Osman dakika ya 81. Ikumbukwe Gor Mahia na Khartoum zilikutana awali na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa Kundi A.
  Robo Fainali nyingine zitachezwa kesho kati ya Al Shandy Sudan dhidi ya KCCA ya Uganda kuanzia Saa 7:45 mchana na baadaye Azam FC dhidi ya Yanga SC, Uwanja huo huo wa Taifa, Dar es Salaam.
  Nusu Fainali zitafuatia Ijumaa na Fainali pamoja na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu itakuwa Jumapili, siku ya kilele cha mashindano hayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: GOR MAHIA YAICHAPA 2-1 MALAKIA, KUKUTANA NA KHARTOUM N TENA NUSU FAINALI IJUMAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top