• HABARI MPYA

  Ijumaa, Julai 31, 2015

  DOGO FARID WA AKADEMI AIPELEKA AZAM FC FAINALI KAGAME, KCCA YAFA 1-0 TAIFA

  Shangwe za shujaa; Farid Malik Mussa akishangilia baada ya kuifungia bao pekee Azam FC leo dhidi ya KCCA 
  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  CHIPUKIZI aliyepandishwa kutoka akademi mwaka juzi, Farid Malik Mussa leo amekuwa shujaa wa Azam FC baada ya kufunga bao pekee lililoiwezesha timu hiyo kutinga Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
  Farid mwenye umri wa miaka 18, alifunga bao hilo dakika ya 76 kwa ustadi wa hali ya juu, baada ya kuruka juu kwenda kuunganisha kwa guu la kushoto krosi ya Ame Ally ‘Zungu’.
  Azam FC sasa itamenyana na Gor Mahia ya Kenya katika fainali Jumapili- hiyo ikiwa ni mara ya pili kwa timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake kufika hatua hiyo, baada ya awali, mwaka 2012 kufungwa na Yanga SC 2-0 Dar es Salaam pia.  
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Suleiman Ahmed wa Djibouti aliyesaidiwa na Yatayew Balachew wa Ethiopia na Nagi Ahmed wa Sudan, kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu.
  Azam FC walipoteza nafasi mbili za kufunga dakika ya tisa Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ akimdakisha kipa wa KCCA, Opio Emmanuel na dakika ya 33 Kipre Herman Tchetche alipiga nje.
  Farid Mussa akimtoka beki wa KCCA leo Uwanja wa Taifa
  Beki wa KCCA, Hassan Wasswa akimzuia mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche asiufikie mpira
  Kiungo wa Azam FC, Mudathir Yahya akipambana na Nahodha wa KCCA, Tom Masiko
  Mshambuliaji wa Azam FC, John Raaphael Bocco akimiliki mpira mbele ya beki wa KCCA
  Beki wa Azam FC, Erasto Nyoni akiwatoka mabeki wa KCCA

  Nafasi nzuri zaidi ambayo KCCA wataijutia kwa kushindwa kuitumia kipindi cha kwanza ilikuwa ni dakika ya 36, baada ya shuti kali la Isaac Sserunkuma kudakwa na kipa wa Azam FC, Aishi Salum Manula.
  Kipindi cha pili, Azam ilikianza kwa mabadiliko, wakimpumzisha kiungo aliyefanya kazi nzuri Mudathir Abbas Yahya na kumuingiza mshambuliaji Ame Ally ‘Zungu’.
  Mabadiliko hayo hakika yaliisaidia Azam FC, kwani iliongeza kasi ya mashambulizi langoni kwa wapinzani na hatimaye baada ya kosakosa kadhaa, Farid akaipeleka timu fainali dakika ya 76.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Aggrey Morris, Serge Wawa, Said Mourad, Erasto Nyoni/Shomary Kapombe dk65, Farid Mussa, Jean Baptiste Mugiraneza, Frank Domayo, Mudathir Yahya/Ame Ally ‘Zungu’ dk46, John Bocco na Kipre Herman Tchetche/Didier Kavumbangu dk75.
  KCCA; Opio Emmanuel, Thom Masiko, Joseph Ochaya, Hassan Wasswa, Dennis Okoth, Muzamiru Mutyaba, Iven Ntege, Hakim Senkuma, Isaac Sserunkuma/Shaaban Kondo dk37, Timoth Awany na Habib Kavuma/Michael Birungi dk81.
  Farid Mussa akishangilia na Said Mourad na Frank Domayo
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: DOGO FARID WA AKADEMI AIPELEKA AZAM FC FAINALI KAGAME, KCCA YAFA 1-0 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top