• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 27, 2015

  KUELEKEA PAMBANO LA YANGA NA AZAM KAGAME; JOHN BOCCO ANAWANYIMA USINGIZI JANGWANI

  Bocco anawanyima usingizi Yanga SC
  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam keshokutwa zitawaka moto kwa pambano kali la Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, baina ya Azam FC na Yanga SC.
  Itakuwa mara ya pili, Yanga SC na Azam FC kukutana katika Kombe la Kagame, baada ya mwaka 2012 kukutana katika fainali pale pale Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.
  Ilikuwa Julai 28, mwaka 2012 katika mchezo uliochezeshwa na refa Thierry Nkurunziza wa Burundi, Yanga SC ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 wafungaji Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 44 na Said Bahanunzi ‘Spider Man’ dakika ya 90 na ushei.
  Sahau kuhusu washambuliaji wengine hatari wa Azam FC kama Kipre Herman Tchetche kutoka Ivory Coast, Didier Kavumbangu wa Burundi na mzalendo Ame Ali- kuna mtu anaitwa John Raphael Bocco.
  Kuelekea mchezo wa Robo Fainali Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kesho kati ya Yanga SC na Azam FC hilo ni gumzo kubwa.
  Mshambuliaji huyo mrefu maarufu kwa jina la utani Adebayor, anaweza asifunge mabao msimu mzima, lakini inapowadia mechi dhidi ya Yanga SC lazima atakwenda kwenye kibendera kushangilia bao.
  Mashabiki wenyewe wa Yanga SC wanaamini beki yao haiwezi kumzuia Bocco kufunga- maana yake hilo ni tishio kweli kwao kuelekea mchezo wa keshokutwa.
  Hadi sasa, Bocco amefunga mabao mawili katika Kombe la Kagame wakati Kipre Tchetche pia ana mabao mawili. Ame hajafunga, lakini ametoa pasi za mabao. 
  Safu ya ulinzi ya Yanga SC ndiyo kongwe kwa sasa Tanzania, ikiundwa na mabeki waliocheza pamoja kwa muda mrefu, Kevin Yondan na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’- ambao wote wameshindwa kuonyesha wanaweza kumdhibiti Bocco katika mechi zilizopita.
  Je, Cannavaro na Yondan sasa wamepata dawa ya kumdhibiti Bocco? Tutajua keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KUELEKEA PAMBANO LA YANGA NA AZAM KAGAME; JOHN BOCCO ANAWANYIMA USINGIZI JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top