• HABARI MPYA

    Saturday, April 18, 2015

    REAL MADRID WAANZA MCHUJO WA VIJANA 500 KUSAKA 30 WA KUNGIA AKADEMI YAO NA NASSF

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MAKOCHA watatu kutoka akademi ya Real Madrid ya Hispania, Royco Garcia, Juanjo San Roman na Francesco Martin leo wameanza kusaka vijana 30 wa kuingia kwenye akademi inayojengwa kwa ushirikiano na Shirika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii la Taifa (NSSF) kutoka kwenye kundi la watoto 500. 
    Zoezi hilo limefanyika asubuhi ya leo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na zaidi ya vijana 50 walikuwa wakifanyiwa usaili na makocha hao vijana.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo wakati wa mchujo huo, Garcia alisema kwamba wamewagawa watoto katika makundi kadhaa na watawafanyia usaili kwa awamu ili kupata vijana 30 wa kuingia akademi. 
    “Tumeanza vizuri, zoezi inaonyesha litakwenda vizuri, ingawa litakuwa gumu kwa sababu kuna vipaji vingi sana,”amesema Garcia ambaye alikuwa akiwafanyia usaili makipa.
    Watoto hao wanatokana msako wa vipaji uliofanyika Dar es Salaam, Unguja na Pembe na Ofisa Uwekezaji wa NSSF, Moringe Magige amsema kwamba awamu ya pili watakwenda mikoa mingine.
    “Kwa sasa tayari tuna vijana 500, ambao tutakuwa tunawaita kwa awamu kufanyiwa usili kusaka wachezaji 30 wa kuingia akademi,”amesema Magige. Kuhusu lini zoezi litakamilika, Magige amesema itategemea na kasi ya walimu hao katika usaili wao. 
    Kocha Juanjo San Roman akiwasaili vijana leo Uwanja wa Karume
    Vijana wakionyesha uwezo wao mbele ya makocha wa Real Madrid
    Kocha Francesco Martin akiwasaili vijana leo Uwanja wa Karume
    Makocha wa Real Madrid wamevutiwa na vipaji vya vijana hawa
    Royco Garcia akiwasaili makipa leo Uwanja wa Karume

    Garcia aliiwakilisha Real Madrid nchini wakati wa kusaini Mkataba na NSSF Februari mwaka huu wa kujenga kituo cha michezo kwa ajili ya kuzalisha vipaji. 
    Katika hafla ya kusaini mkataba huo wa miaka 18, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhani Dau alisema ujenzi huo utagharimu Sh Bilioni 16 na unatarajiwa kuanza Mei mwaka huu na kwamba utakamilika baada ya miezi 18.
    Dk Dau alisema kituo hicho kitajengwa kwenye kijiji cha michezo cha shirika hilo kikijulikana kama NSSF Sports City, eneo la Mwasonga, Kigamboni, Dar es Salaam. 
    “Tuna eneo la zaidi ya ekari 400 ambapo tutajenga viwanja, shule ya michezo, nyumba za kuishi na maduka. Lengo letu tuzalishe na kuuza wachezaji. Tunakusudia kuwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 13, 18, 20, timu B na timu ya wakubwa,” alisema Dk Dau. 
    Alisema utekelezaji wa kituo hicho utaanza hivi karibuni kwa kutumia majengo ya kukodi wakati wakisubiri ujenzi kukamilika.“Hivi hapa baada ya kusaini mkataba, utekelezaji utaanza kwa kutumia majengo ya kukodi ambayo tunadhani yatakuwa maeneo ya Temeke na tutakuwa tukitumia viwanja vya Karume na Uhuru,” alisema. 
    Mkurugenzi Mkuu huyo wa NSSF alisema katika kuendesha kituo hicho, kila kitu kitafanywa na Real Madrid kuanzia masuala yote ya ufundi, kuwatambua wachezaji, chakula, wataalamu wa saikolojia na wataalamu wa viungo na kwamba wajibu wa shirika lake utakuwa kwenye kujenga tu. 
    “Sisi tunachukulia huu mradi ni uwekezaji na hatufanyi hisani, itazingatia misingi ya biashara na faida kubwa ni kwamba NSSF itaongeza kipato, lakini pia kituo kitatumika kuitangaza Tanzania kwa sababu yatakayofanyika yataonyeshwa kwenye Televisheni ya Real Madrid,” alifafanua Dk Dau. 
    “Lakini pia wakati umefika sasa kwa Tanzania kushiriki Kombe la Dunia Qatar 2022, kama unaandaa vizuri vijana wa miaka 13 sasa mpaka mwaka 2020 wanaweza kuwakilisha vizuri kwenye mechi za kufuzu na mwaka 2022 wakashiriki Kombe la Dunia, wakikosa la Qatar, basi hata hizo zinazokuja, hiyo pia ni moja ya madhumuni ya kituo hicho.” 
    Akizungumzia namna walivyofikia uamuzi wa kujenga kituo, Dk Dau alisema wazo hilo lilipatikana Agosti mwaka jana na kisha likapelekwa kwenye Mkutano wa Wanachama uliofanyika Arusha ambako waliazimia NSSF iwekeze rasmi kwenye michezo kabla ya kuwasilishwa kwenye bodi na utekelezaji kuanza kufanyika. 
    “Tulitembelea sehemu nyingi kuona wenzetu wanafanyaje. Binafsi nilitembelea nchi kadhaa za Ulaya, nilienda kituo cha Manchester United, Sunderland, Real Madrid kwa hapa Afrika nilikwenda Asec Mimosas (Ivory Coast) na TP Mazembe (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC) kuona wanafanyaje, ziara ikazaa matunda kwani tulikubaliana na Madrid,” alifafanua Dk Dau. 
    Mradi huu ni matunda ya ziara ya kikosi cha magwiji wa Real Madrid waliozuru nchini Agosti mwaka jana wakiongozwa na Mwanasoka Bora wa zamani wa dunia, Mreno Luis Figo na kucheza mechi ya kirafiki na wachezaji nyota wa zamani wa Tanzania.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: REAL MADRID WAANZA MCHUJO WA VIJANA 500 KUSAKA 30 WA KUNGIA AKADEMI YAO NA NASSF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top