• HABARI MPYA

    Friday, April 06, 2018

    SIMBA SC KUWAKOSA KOTEI, JUUKO NA NYONI MECHI NA MTIBWA SUGAR JUMATATU MOROGORO

    Na Princess Asia DAR ES SALAAM
    SIMBA SC itawakosa wachezaji wake watatu, mabeki Mganda Juuko Murshid, mzawa Erasto Nyoni na kiungo Mghana, James Kotei katika mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Mtibwa Sugar Jumatatu Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kutokana na kutumikia adhabu ya kadi za njano.
    Lakini kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre anajivunia kurejea kwa, Jonas Gerald Mkude aliyepona maumivu ya kifundo chake cha mguu alichoumia wiki mbili zilizopita mazoezini mjini Dar es Salaam baada ya kugongana na mchezaji mwenzake, Muzamil Yassin.
    Erasto Nyoni (kushoto) na James Kotei (kulia) watakosekana dhidi ya Mtibwa Sugar Jumatatu sababu ya kadi za njano 

    Pamoja na kadi tatu za njano, lakini pia Kotei anayeweza kucheza na nafasi za ulinzi pia, alishindwa kuendelea na mchezo Jumanne wiki hii Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe, Simba SC ikishinda 2-0 dhidi ya wenyeji, Njombe Mji FC baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Salim Mbonde.
    Simba imeweka mkoani Iringa tangu juzi ikitokea Njombe na leo mapema inatarajiwa kuondoka kwenda Morogoro kwa ajili ya mchezo wake ujao Uwanja wa Jamhuri Jumatatu.
    Na Lechantre amesema kikosi chake kipo vizuri, hakuna majeruhi na huenda akamtumia Mkude kulingana na maendeleo yake katika mazoezi ya kujiandaa na mchezo huo.
    Alisema anahitaji pointi tatu muhimu kwa michezo iliyobakia ikiwemo dhidi ya Mtibwa Sugar wanaocheza Jumatatu na dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Alhamisi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    “Hizi ni mechi muhimu sana kwetu, tunahitaji pointi sita kabla ya kucheza na Yanga. Umakini ni muhimu kwa wachezaji wangu katika kila idara. Tutawakosa wachezaji watatu lakini pia kuna watu watachukua nafasi zao,” alisema Lechantre.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC KUWAKOSA KOTEI, JUUKO NA NYONI MECHI NA MTIBWA SUGAR JUMATATU MOROGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top