• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 21, 2018

  SIMBA SC YAPUNGUZWA KASI, SARE 1-1 TENA NA LIPULI SAMORA

  Na Mwandishi Wetu, IRINGA
  TIMU ya Simba SC imepunguzwa kasi baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Lipuli FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Samora mjini Iringa leo.
  Pamoja na sare hiyo, Simba SC inaendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifikisha pointi 59 baada ya kucheza mechi ya 25, mbele ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 47 za mechi 22, wakati Lipuli inafikisha pointi 32 katika mechi ya 26 na kupana kwa nafasi moja kutoka ya nane, ikiishusha Ruvu Shooting.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hanc Mabena wa Tanga, aliyesaidiwa na Rashid Abdallah na Rashid Zongo Lipuli ilimaliza kipindi cha kwanza ikiwa inaongoza kwa bao 1-0. 
  Bao hilo lilifungwa na Mchezaji Bora wa Ligi Kuu kwa mwezi Machi, Adam Salamba dakika ya 31, aliyemlamba chenga beki Yussuf Mlipili kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa namba moja Tanzania, Aishi Manula.
  Bao hilo lilionekana kuwavuruga kidogo Simba SC na kuwaruhusu Lipuli FC kutawala zaidi mchezo, lakini Wana Paluhengo wakashindwa kutumia mwanya huo kupata mabao zaidi.
  Kipindi cha pili, kocha Mfaransa wa Simba SC, Pierre Lechantre alikianza na mabadiliko, akimtoa beki Juuko Murshid na kumuingiza mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo ambaye alikwenda kuiongezea uhai safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
  Mavugo, aliye katika msimu wake wa pili Simba SC tangu asajiliwe kutoka Vital’O ya kwao, aliifungia SImba SC bao la kusawazisha dakika ya 66 baada ya kona iliyochongwa na beki Shomary Salum Kapombe.
  Mpira wa Kapombe ulikwenda moja kwa moja kwenye kichwa cha Erasto Nyoni aliyeunganisha, lakini ukamgonga beki wa Simba, Mghana Asante Kwasi aliyekuwa amesimama kwenye mstari wa lango la Lipuli na kurudi ndani pembeni kulia, ambako ulimkuta Mavugo aliyefunga.
  Baada ya bao hilo, Simba SC ilicharuka na kuongeza mashambulizi langoni mwa Lipuli kusaka bao la ushindi, lakini safu ya ulinzi ya Wana Paluhengo ikiongozwa na beki Mganda, Joseph Owino ilisimama imara kudhibiti hatari zote. Mechi ya kwanza, Jumapili ya Novemba 26, Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya 1-1 pia.
  Kocha Mkuu wa Simba SC, Suleiman Matola kipindi cha pili alionekana akizozana na Meneja wa timu hiyo, Mrisho Gambo. Baadaye Matola akasema alikuwa anamzuia Meneja huyo kuingilia kazi yake ya kuwaelekeza wachezaji.  
  Baada ya mchezo huo, Simba SC inarejea Dar es Salaam kuanza maandalizi ya mchezo wake ujao dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga Aprili 29, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kikosi cha Lipuli FC kilikuwa; Mohammed Yussuf, Steven Mganga, Paul Ngalema, Ally Mtoni, George Owino, Fred Tangalu, Daruwish Saliboko, Mussa Nampaka, Adam Salamba, Malimi Busungu na Seif Karihe. 
  Simba SC; Aishi Manula, Nicholaus Gyan, Asante Kwasi, Juuko Murshid/Laudit Mavugo dk46, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei, Shomary Kapombe, Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAPUNGUZWA KASI, SARE 1-1 TENA NA LIPULI SAMORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top