• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 28, 2018

  SAMATTA ACHEZA DAKIKA 20 TU, GENK YALAZIMISHWA SARE 1-1 NYUMBANI

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa kuamkia leo amecheza kwa dakika 20 na ushei, klabu yake, KRC Genk ikilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Club Brugge katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
  Samatta jana alianzia benchi na Genk wakatanguliwa kwa bao la mshambuliaji Mbrazil, Moraes Ferreira da Silva, maarufu kama Wesley aliyefunga dakika ya 65 akimalizia pasi ya Mfaransa Abdoulay Diaby.
  Dakika moja kabla ya Samatta kuinuliwa kwenda kuchukua nafasi ya mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos KarellisGenk ikapata bao la kusawazisha dakika ya 69.
  Mbwana Samatta akimtoka mchezaji wa Brugge jana baada ya kuingia dakika 20 za mwisho

  Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Mbelgiji, Leandro Trossard dakika ya 69, akimalizia kazi nzuri ya kiungo kutoka Angola, Clinton Mukoni Mata Pedro Lourenco, maarufu tu Clinton Mata. 
  Samatta jana amecheza mechi ya 85 tangu Nahodha huyo wa Taifa Stars ajiunge na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 
  Na katika mechi hizo, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano yote.
  Kikosi cha KRC Genk kilikuwa: Vukovic, Nastic, Colley, Aidoo, Mata/Maehle dk83, Wouters, Seck, Malinovskyi, Pozuelo, Trossard na Karelis/Samatta dk70.
  Club Brugge; Gabulov, Poulain, Wesley, Diaby/Dennis dk86, Diatta, Limbombe/Cools dk87, Vanaken/Clasie dk84, Denswil, Vormer, Nakamba na Mechele
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA ACHEZA DAKIKA 20 TU, GENK YALAZIMISHWA SARE 1-1 NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top