• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 21, 2018

  SIMBA SC KUIKANDAMIZA LIPULI LEO SAMORA LEO?

  Na Mwandishi Wetu, IRINGA
  VINARA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC leo wanateremka Uwanja wa Samora mjini Iringa kumenyana na wenyeji, Lipuli FC katika mwendelezo wa mawindo yao ya taji la kwanza la ubingwa wa michuano hiyo tangu mwaka 2012.
  Simba inateremka Uwanja wa Samora leo, ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa na sare ya 1-1 na Wana Paluhengo Jumapili ya Novemba 26, Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Na safari hii, makocha wa Lipuli FC, Suleiman Matola na Amri Said ambao wote ni wachezaji wa zamani wa Simba, tena waliojifunzia ualimu wa mpira katika klabu hiyo wametamba kuifunga timu yao hiyo ya zamani. 
  Kwa upande wake, Kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anaumiza kichwa juu ya kipa Aishi Salum Manula na mshambuliaji Emmanuel Arnold Okwi kuwachezesha au kutowachezesha leo. 
  Wawili hao, kipa namba moja wa Tanzania na mshambuliaji tegemeo wa Uganda kila mmoja tayari ameonyeshwa kadi mbili za njano na kama atawachezesha kesho na bahati mbaya wakaonyeshwa tena kadi, maana yake watakosekana kwenye mechi dhidi ya mahasimu, Yanga Aprili 29, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Lakini wakati huo huo wawili hao wamekuwa muhimu mno katika kampeni za Simba SC kutwaa taji la kwanza la ubingwa wa Ligi Kuu baada ya miaka sita na Lechantre anayesaidiwa na Mtunisia, Aymen Mohammed Hbibi, Mrundi Masoud Juma na mzawa, Muharami Mohammed ‘Shilton’ anahofia kuwatumia huku akihitaji kuwatumia.
  Kipa wa pili, Said Mohammed ‘Nduda’ aliyesajiliwa msimu huu kutoka Mtibwa Sugar yupo fiti, lakini hajadaka mechi hata msimu huu ukiondoa ile ya kirafiki dhidi yake hiyo ya zamani kutoka Manungu, Turiani mkoani Morogoro Agosti 13, mwaka jana Uwanja wa Taifa.
  Na Okwi ndiye amekuwa injini ya Simba SC akiwa amefunga mabao 19 msimu huu katika Ligi Kuu pekee, akiisaidia timu hiyo kuwa kileleni kwa pointi zake 58 za mechi 24, mbele ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 47 za mechi 22.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUIKANDAMIZA LIPULI LEO SAMORA LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top