• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 22, 2018

  MTIBWA SUGAR: TUMEMALIZA ADHABU CAF, TUKIWA MABINGWA ASFC TUTASHIRIKI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Mtibwa Sugar ya Morogoro imesema kwamba itashiriki michuano ya Afrika mwakani ikifuzu, kwa sababu adhabu yao ilikwishamalizika.
  Hayo yamesemwa na Katibu Msaidizi wa timu hiyo, Abubakar Swabur leo alipozuzungumza na Bin Zubeiry Sports – Online mjini Dar es Salaam, kufuatia imani iliyopo kwamba Mtibwa Sugar haitashiriki michuano ya Afrika hata ikifuzu. 
  “Kumekuwepo na propaganda za kwamba Mtibwa Sugar haitashiriki michuano ya kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la soka Afrika (CAF), propaganda hizi ni za uongo za inabidi zipuuzwe kabisa hazina ukweli wowote. Ni kweli Mtibwa Sugar ilifungiwa miaka mitatu na kupigwa faini ya fedha juu mwaka 2004,”. 
  Swabur alisema kwamba faini waliilipa kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kwa hesabu za haraka walimaliza adhabu yao ya kufungiwa miaka mitatu mwaka 2007 na kwamba wako huru kucheza michuano ya Afrika tangu mwaka 2008.
  “Propaganda hizi zinasema  Mtibwa Sugar haiwezi kushiriki kutokana kwamba ile adhabu  unaanza kuitumikia iwapo klabu itafuzu michuano hiyo na Mtibwa Sugar haijawahi kufuzu michuano hiyo tangu ifungiwe, hivyo haiwezi kushiriki michuano hiyo hadi ifuzu tena mara mbili bila kucheza ili kutumikia adhabu yao”,
  Swabur ameongeza; “Haya si kweli, yanalenga kuwatoa katika reli wana Mtibwa Sugar ambao wamekuja na kauli mbiu ya heshima, ambayo inasema "Heshima ya 1999-2000  irejee".  Ukweli ni kwamba timu yeyote ikifungiwa kutokana na michuano inayoratibiwa na CAF inafungiwa miaka na timu  inaanza kutumikia adhabu hiyo baada ya kupokea taarifa hiyo na haisubiri hadi ikifuzu kwa maana nyingine adhabu hiyo siyo lazima ufuzu ndiyo uitumikie,”. 
  “Kwa wanasheria kuna kitu kinaitwa ‘precedent’ kwa maana nyingine, kesi zenye mazingira yanayofanana. Kwa suala la Mtibwa Sugar naomba nije na precedent au kesi zinazofanana na hukumu iliyotolewa na CAF kwa Mtibwa Sugar,”
  “Highlanders ya Zimbabwe ilifungiwa na CAF miaka mitatu  kwa kushindwa kusafiri kucheza na Nchanga Rangers ya Zambia na adhabu hiyo walianza kuitumikia mwaka 2012 na baada ya miaka miwili Highlanders kupitia ZIFA (Shirikisho la Soka Zimbabwe) wakaomba kupewa msamaha, CAF waliwajibu adhabu inaisha mwaka 2015, wavumilie,”
  “Mwaka 2012, Abeid Pele na timu yake ya Nania Fc ya Ghana walifungiwa miaka mitatu na kupigwa faini ya dola za Kimarekanio 1,500 na CAF walionyesha adhabu hiyo inaisha mwaka 2016, hivyo CAF walikuwa wanajua hawa jamaa watafuzu mara zote, au?,” 
  “Keizer Chiefs ya Afrika Kusini nayo mwaka 2004 ilifungiwa miaka mitatu na kupigwa faini ya dola 1,500 kwa kushindwa kusafiri kwenda kucheza mchezo wa marudiano na Esperance ya Tunisia baada ya kufungwa mchezo wa kwanza nyumbani. Na wakati adhabu yao inaisha walikuwa nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu Afrika Kusini, ambayo haiwapi fursa ya kushiriki michuano hiyo ya kimataifa na adhabu yao ilimalizika wakiwa hawapo kwenye nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa,”amesema Swabur.
  Kiongozi huyo amessema kwamba Mtibwa Sugar inajipanga kikamilifu kwa mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) Juni 2, mwaka huu Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, ambayo wakifuzu watapata tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR: TUMEMALIZA ADHABU CAF, TUKIWA MABINGWA ASFC TUTASHIRIKI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top