• HABARI MPYA

    Thursday, April 26, 2018

    SIMBA SC YAWATANGULIA YANGA DAR, YAENDA KUJICHIMBIA PEMBEZONI MWA BAHARI YA HINDI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC tayari wapo mjini Dares Salaam tangu mchana kwa maandalizi ya mwisho ya pambano dhidi ya mahasimu wao, Yanga SC Jumapili Uwanja wa Taifa.
    Baada ya mazoezi yao asubuhi tu Uwanja wa Highland, Morogoro, wachezaji wa Simba na benchi lao zima la ufundi wakapanda basi lao kurejea Dar es Salaam ambakio wamefikia katika hoteli ya SeaScape, eneo la Mbezi Beach, pembezoni mwa Bahari ya Hindi.
    Simba SC ilikuwa Morogoro tangu Jumapili kwa kambi ya maandalizi ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu, Yanga Jumapili,
    Iliwasili Morogoro ikitoka Iringa ambako Jumamosi ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Lipuli FC katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu.
    Kocha Mfaransa, Pierre Lechantre (kushoto) akiwa na Msaidizi wake namba moja, Mtunisia, Aymen Mohamed Hbibi (kulia)

    Watani wao, Yanga nao wapo Morogoro tangu Jumatatu, siku moja tu baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, Mbeya City katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Uwanja wa Sokoine.
    Matarajio ni Yanga SC ambao ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu kuingia Dar es Salaam mapema kesho tayari kwa mchezo huo wa Jumapili.
    Jumapili inagarajiwa kuwa siku kubwa mno katika soka ya Tanzania, miamba hiyo ya soka nchini ikimenyana vikali katika mbio za ubingwa.
    Simba SC iliyo chini ya kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mtunisia, Aymen Mohamed Hbibi, Mrundi, Masoud Juma na mzawa Muharami Mohamed ‘Shilton’ inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 59 baada ya kucheza mechi 25, wakati Yanga inafuatia kwa mbali kidogo ikiwa na pointi zake 48 za mechi 23.
    Yanga inazidiwa pointi 11 na Simba SC na ina viporo viwili, maana yake ili kutetea ubingwa wao, itabidi washinde Jumapili na washinde mechi zao zote zilizobaki za Ligi Kuu, huku wakiwaombea mahasimu wao hao wapoteze mechi nyingine pia moja – jambo ambalo hakika ni gumu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAWATANGULIA YANGA DAR, YAENDA KUJICHIMBIA PEMBEZONI MWA BAHARI YA HINDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top