• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 28, 2018

  AZAM FC YAISHUSHA YANGA SC HADI NAFASI YA TATU, MAJI MAJI YANG’ARA SONGEA

  Na Mwandishi Wetu, TURIANI
  BAO pekee la mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda dakika ya 43 limeipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mtbwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
  Ushindi huo, unaifanya Azam FC ifikishe pointi 49 baada ya kucheza mechi 26 na kupanda hadi nafasi ya pili, ikiwashushia nafasi ya tatu, mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 48 za mechi 23.
  Simba SC ambayo kesho itamenyana na mahasimu wao wa jadi, Yanga SC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 59 za mechi 25. 
  Shaaban Iddi (katikati) amefunga bao pekee leo Azam FC ikishinda 1-0 dhidi ya Mtbwa Sugar 

  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Maji Maji ya Songea imepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting Stars katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Maji Maji mjini Songea.
  Kwa ushindi huo, Maji Maji inafikisha pointi 23 baada ya kucheza mechi 26 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya 14 katika Ligi Kuu ya timu 16, wakati Ruvu inabaki nafasi ya nane kwa pointi zake 32 za mechi 26 pia. 
  Nayo Stand United imegawana pointi moja moja na Kagera Sugar ya Bukoba baada ya sare ya 0-0 katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  Kagera Sugar ya kocha Mecky Mexime, inafikisha pointi 27 za mechi 26 na inapanda kwa nadasi moja hadi ya 11, wakati Stand United inafikisha pointi 29 baada ya kucheza mechi 26 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya tisa.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAISHUSHA YANGA SC HADI NAFASI YA TATU, MAJI MAJI YANG’ARA SONGEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top