• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 29, 2018

  MSUVA AFUNGA LA KWANZA DIFAA HASSAN EL-JADIDA YASHINDA 5-2 LIGI YA MOROCCO

  Na Mwandishi Wetu, MARRAKECH
  WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva usiku wa jana amefunga bao moja, timu yake, Difaa Hassan El- Jadida ikiibuka na ushindi wa 5-2 dhidi ya wenyeji, Kawkab Marrakech katika mchezo wa Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kama Botola Pro uliofanyika Uwanja wa Marrakech.
  Msuva, Mfungaji Bora na Mchezaji Bora wa zamani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara akiwa na klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, alifungua shangwe za mabao kwa bao lake zuri dakika ya 10 tu mbele ya mashabiki wengi wa wenyeji.
  Adnane El Quadry akafunga la pili dakika ya 16, Fabrice Ngah akafunga la tatu dakika ya 70, Ayoub Nanah akafunga la nne dakika ya 86 na Bilal El Magri akafunga la tano dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida.
  Mabao ya wenyeji, Kawkab Marrakech yalifungwa na Yassine Dahbi yote mawili dakika za nne na 45 katika mchezo huo ambao Msuva alimpisha El Hasnaoui dakika ya 84.
  Simon Msuva jana amefunga bao moja, Difaa Hassan El- Jadida ikishinda 5-2 dhidi ya Kawkab Marrakech
  Ushindi huo, unaipeleka Difaa Hassan El-Jadida nafasi ya pili kwenye msimamo wa Botola Pro ikifikisha pointi 44 baada ya kucheza mechi 27, ikiwa nyuma ya vinara, Ittihad Tanger wenye pointi 47 za mechi 26 na mbele ya mabingwa wa Afrika, Wydad Casablanca wenye pointi 43 za mechi 26.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MSUVA AFUNGA LA KWANZA DIFAA HASSAN EL-JADIDA YASHINDA 5-2 LIGI YA MOROCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top